RC CHALAMILA ATANGAZA MSAKO MKALI DHIDI YA MATAPELI WA ARDHI DAR, AWAALIKA WANANCHI KUWASILISHA USHAHIDI
Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza operesheni maalum ya kukomesha vitendo vya uporaji wa ardhi na utapeli vinavyolalamikiwa kukithiri katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo. Ametoa muda wa wiki moja kuanzia Machi 2, 2026 kwa wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kujisalimisha na kurejesha mali walizozichukua isivyo halali kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya ziara yake Wilaya ya Kinondoni, RC Chalamila alisema serikali imebaini ongezeko la malalamiko yanayohusu uporaji wa ardhi, unyang’anyi wa mali na udanganyifu wa mikataba ya upangishaji. Alieleza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakikodisha maeneo kwa njia za ujanja kisha kuyageuza kuwa mali zao kwa hila, jambo linalosababisha migogoro na maumivu kwa wahanga.
Aidha, amegusia utapeli unaodaiwa kufanyika katika baadhi ya maduka ya kuuzia magari (showroom), ambapo wananchi hulipia magari lakini hukosa kuyapata kwa kisingizio cha kwamba bado yapo bandarini. Pia alionya juu ya mikopo yenye masharti kandamizi inayodaiwa kuwaumiza wananchi, akisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na hatua zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
RC Chalamila amewataka wananchi wote waliotapeliwa au kudhulumiwa mali zao kuwasilisha malalamiko rasmi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ndani ya muda wa wiki moja kuanzia Machi 2, 2026. Amesema kuanzia Machi 9 ataanza ziara maalum ya kushughulikia migogoro hiyo kwa lengo la kurejesha haki kwa waathirika.
Katika hatua nyingine, ameipongeza Mahakama pamoja na TAKUKURU kwa juhudi zao katika kushughulikia kesi za aina hiyo. Hata hivyo, ametoa onyo kwa baadhi ya wasimamizi wa mirathi wanaotumia vibaya nafasi zao kwa kuuza mali za warithi kwa visingizio mbalimbali, akisema serikali haitavumilia vitendo vya kunyima warithi haki zao.
Wakati huo huo, RC Chalamila amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi Machi 3, 2026 kumpokea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anayetarajiwa kuzindua matanki ya kuhifadhia mafuta katika Wilaya ya Kigamboni. Amesema ujio huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu ya nishati na kukuza uchumi wa mkoa huo.
RC Chalamila pia ametoa wito kwa wananchi kutojihusisha na migogoro ya ardhi kwa njia zisizo rasmi, bali kufuata taratibu za kisheria na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kukomesha tatizo hilo kwa pamoja.
Katika hatua nyingine, RC Chalamila ametoa wito kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga kujiepusha na kufanya biashara pembezoni mwa barabara, akisisitiza kuwa maeneo hayo yanapaswa kuachwa wazi ili kuruhusu upanuzi wa barabara na kurahisisha usafiri kulingana na hadhi ya jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 2, 2026, amesema hafukuzi machinga bali anawataka kuacha kufanya biashara barabarani na badala yake waende katika Soko Kuu la Kariakoo ili kuendelea na shughuli zao katika mazingira rasmi, salama na yenye mpangilio mzuri.


Hakuna maoni: