IDP YAWAJENGEA UWEZO WAANDISHI WA HABARI KUHAMASISHA KILIMO IKOLOJIA TANZANIA



Arusha.

Kuongeza uelewa wa jamii kuhusu kilimo ikolojia ni changamoto inayohitaji mshikamano wa wadau mbalimbali, hususan waandishi wa habari. Hii ni hoja iliyothibitishwa katika warsha maalumu iliyofanyika Arusha, iliyojumuisha mafunzo na mijadala ya kina kuhusu kilimo hai na mbinu za asili za uzalishaji wa chakula.

Warsha hiyo iliyoandaliwa na shirika la Iles de Paix (IDP) ililenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuhamasisha kilimo ikolojia nchini Tanzania, huku ikiweka msisitizo kwenye uhusiano wa jamii na uzalishaji endelevu wa chakula.

Mkurugenzi wa IDP, Ayesiga Buberwa,
akizungumza wakati wa warsha hiyo, amesema:
“Tunataka kuhakikisha jamii nzima inahusika katika kilimo hai. Ndiyo maana tunawaita waandishi wa habari ili kutoa elimu na kujengeana uzoefu ambao utasaidia kuelimisha wananchi kwa upana wake.”

Kauli hii inasisitiza lengo kuu la shirika la kuendeleza mifumo kamili ya uzalishaji wa chakula kwa njia salama, huku waandishi wa habari wakiwa kiungo muhimu katika kueneza elimu na uhamasishaji wa kilimo ikolojia.


IDP YAFANYA KAZI KUBWA KATIKA KILIMO IKOLOJIA

Shirika la IDP linafanya kazi katika nchi mbalimbali duniani, likishirikiana na mashirika ya ndani, vyuo vikuu, Taasisi za serikali na sekta binafsi. Katika Tanzania, linafanya kazi kwa karibu na Chuo cha Nelson Mandela na Sokoine, pia Shirika limekuwa likishirikiana na taasisi mbalimbali, zikiwemo:

⦿ Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Mkoa wa Arusha (MVIWAARUSHA)

⦿ Research Community and Organizational Development Associates (RECODA)

⦿ Shirikisho la Vyama vya Wakulima Wadogo Tanzania (SHIWAKUTA) huku likiendesha miradi katika mikoa ya Simanjiro, Longido, Karatu, na Arusha DC.

Meneja Miradi wa IDP, Linda Temba, amesema:-
“Tunataka kuhakikisha jamii nzima inahusika katika kilimo hai. Ndiyo maana tunawaita waandishi wa habari ili kutoa elimu na kueneza uzoefu unaosaidia wananchi kuelewa kilimo ikolojia kwa upana wake.”

Tangu kuanzishwa mwaka 2015, shirika limefanikisha miradi nane ya kilimo endelevu:

⦿ Maisha Bora (2015–2020)
⦿ Kilimo Endelevu (2017–2021)
⦿ Kilimo Endelevu+ (2021–2023)
⦿ Kilimo Endelevu Arusha (2022–2026)
⦿ Kilimo Endelevu Arusha + (2023–2026)
⦿ Maji kwa Chakula (2023–2024)
⦿ ECO Food Project (2025–2026)
⦿ Agro Kilimo Project (2025–2026)


CHANGAMOTO KATIKA KILIMO IKOLOJIA
Miongoni mwa changamoto zinazokabili kilimo ikolojia ni pamoja na:

⦿ Wakulima kuchukua muda kuelewa na kukubali mbinu za kilimo ikolojia.

⦿ Kutokuwa na sera za kilimo ikolojia zinazorahisisha utekelezaji.

⦿ Upatikanaji mdogo wa masoko ya uhakika kwa mazao ya ikolojia.

⦿ Wakulima, hususan wanawake, kukosa maeneo ya kulima.

⦿ Uchache wa wajasiriamali wa kilimo ikolojia.


Hata hivyo, kilimo ikolojia kimeanza kupenya katika masikio ya wakulima na wananchi, na ni muhimu kuendelea kuzungumzia mifumo thabiti ya matumizi ya mbegu za asili na mbinu za asili badala ya kemikali.


ELIMU KWA JAMII

Afisa wa kilimo ikolojia, Emmanuel Kasemba, ameeleza kanuni kumi muhimu ambazo ni miongozo ya kuendesha kilimo endelevu na kilimo hai:
Ustahimilivu wa mazingira – Kilimo kinafaa kulingana na hali ya asili, kuhusiishe rasilimali na kudumisha ardhi, maji, na misitu. Kama vile mbolea za samadi,mabaki ya mimea nk.

Muunganiko/mseto wa mbegu – Kutumia mbegu mbalimbali na mchanganyiko wa mazao kunasaidia kupunguza hatari za magonjwa na kuimarisha uzalishaji.

Aina mbalimbali za mazao – Kuelimisha wakulima kupanda mazao tofauti kunasaidia kuongeza lishe na kuzuia upungufu wa chakula.

Urejeleshaji wa ardhi – Kutunza na kurejesha rutuba ya ardhi bila kutumia kemikali hatarishi.

Ubinadamu na maadili ya jamii – Kilimo kiendelee kwa kuzingatia maadili ya jamii, kushirikiana, na kuheshimiana.

Utamaduni na chakula – Hali ya kilimo hai inapaswa kuhifadhi utamaduni wa chakula na mbinu za asili za kutunza mazao.

Uchumi wa wote – Kilimo endelevu kinafaida kwa jamii yote, hakitenganii kundi moja pekee, bali kinasaidia kuwa na uchumi thabiti.

Uongozi bora – Kila mradi au shamba linafaa kuendeshwa kwa uwazi, ushirikiano, na uwajibikaji.

Kutegemeana – Wakulima wanashirikiana, kusaidiana, na kujenga mtandao wa msaada wa kilimo.

Kushirikishana maarifa – Ujuzi, mbinu bora, na teknolojia zinapaswa kushirikishwa kati ya wakulima, jamii, na wadau wa kilimo.


MATARAJIO YA BAADAYE

IDP inalenga kuendelea kupeleka elimu kwa wadau na wananchi, kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika, kushawishi sera bora za kilimo ikolojia, na kuwawezesha wanawake na vijana.

 “Hatupo salama kutokana na vyakula tunavyokula. Ni lazima kubadili mifumo ya uzalishaji wa chakula kwa kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Buberwa.

Baada ya Warsha hiyo Waandishi wa habari pia watapata fursa ya kufanya ziara katika maeneo ya utekelezaji wa miradi hiyo iliyopo Karatu, na Arusha Dc ili kuweza kukifahamu kwa undani zaidi kilimo ikolojia.

Ziara ya Arusha ni sehemu ya mkakati wa IDP wa kuunganisha warsha, mashamba, na sokoni ili kupata picha kamili ya kilimo ikolojia nchini, kutoka uzalishaji hadi soko la mwisho.



Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.