ZAIDI YA SPISHI 100 ZA MITI YA ASILI ZATAMBULIWA, WANUFAIKA 1,300 WANUFAIKA NA MRADI WA TFS

Dodoma, Machi 2026

Tanzania imepiga hatua katika juhudi za kurejesha uoto wa asili baada ya kukamilika kwa mradi uliowezesha kutambuliwa kwa zaidi ya spishi 100 za miti ya asili na kuwafikia wanufaika zaidi ya 1,300 nchini.

Mradi huo wa miaka miwili uliotekelezwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Botanic Gardens Conservation International (BGCI) na wadau wengine, ulilenga kuongeza upatikanaji na matumizi ya mbegu za miti ya asili kwa ajili ya kurejesha misitu iliyoharibiwa na kuimarisha bioanuwai.

Kupitia mradi huo uliofadhiliwa na Darwin Initiative ya Uingereza, wataalamu waliandaa pia miongozo ya uzalishaji kwa angalau spishi 30 za kipaumbele, hatua inayotarajiwa kurahisisha upandaji na urejeshaji wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Akizungumza katika warsha ya kuhitimisha mradi huo iliyofanyika Dodoma, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Mbegu za Miti TFS, Dkt. Hamza Katety, alisema mradi umeongeza uwezo wa kitaalamu kwa watumishi na wadau wa sekta ya misitu, hususan katika mnyororo wa thamani wa mbegu kuanzia ukusanyaji hadi uoteshaji.

“Mbali na kuwafikia zaidi ya wanufaika 1,300, mradi umejenga msingi imara wa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za miti ya asili kwa ajili ya urejeshaji wa misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Meneja wa Baiolojia ya Mbegu za Miti kutoka TFS, Fandey Mashimba, alisema matokeo ya mradi tayari yanaanza kuingizwa katika maboresho ya sera, ikiwemo mchakato wa kuandaa kanuni za usimamizi wa mbegu za miti ili kuongeza matumizi ya spishi za asili.

Mradi huo ulitekelezwa kwa ushirikiano na Tanzania Tree Growers Association Union (TTGAU), Bustani ya Mimea ya Migombani Zanzibar na ECHO Impact East Africa, huku ukihusisha pia tafiti za kisayansi za mimea katika kanda mbalimbali za kiikolojia zilizosaidia kuboresha takwimu za kitaifa na upangaji wa urejeshaji wa mazingira.

Naye Meneja wa Uhifadhi wa BGCI Kanda ya Afrika, Roniance Adhiambo, alisema ushirikiano huo una mchango mkubwa katika kufikia malengo ya kimataifa ya urejeshaji wa ardhi, ikiwemo mpango wa AFR100, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza uwekezaji katika spishi za miti ya asili.

Mradi huo unatarajiwa kuacha urithi wa mifumo imara ya uzalishaji wa mbegu, ongezeko la utaalamu na matumizi mapana ya miti ya asili, hatua itakayosaidia kuharakisha juhudi za kurejesha misitu na kulinda mazingira nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.