Na: OWM-KAM,
Morogoro.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Mhe. Rahma Kisuo, amewataka wamiliki wa viwanda kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa ili kulinda maslahi ya wafanyakazi.
Amesema hayo leo Machi 13, 2026, wakati wa ziara yake mkoani Morogoro alipotembelea na kukagua kiwanda cha 21st Century Textile Limited pamoja na Carankali Recycling Tanzania Limited.
Aidha, Mhe. Kisuo amesisitiza kuwa ustawi wa wafanyakazi ni msingi wa maendeleo ya viwanda na uchumi wa Taifa, hivyo amewataka waajiri kuzingatia sheria ili kulinda wafanyakazi wao.
Vilevile, amewataka wafanyakazi kuhakikisha wanatumia vifaa kinga ili kujikinga dhidi ya madhara yatokanayo na ajali wakiwa kazini.
Kwa upande mwengine, Mhe. Kisuo ameiagiza taasisi mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa wafanyakazi ili kuhakikisha elimu hiyo inatolewa inasaidia kuzuia migogoro sehemu za kazi. Pia, amehamasisha Maafisa Kazi kutoa elimu kuhusu maana ya kima cha chini cha mshahara.
Kadhalika, Mhe. Kisuo ameitaka Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kufanya kaguzi za kina katika maeneo ya kazi ili kubaini viwango vya usalama kwa wafanyakazi katika maeneo ya kazi na kuwasilisha ripoti.

Hakuna maoni: