TGC INAVYOBADILI AICC NA KIA MAJUKWAA YA KIMATAIFA YA UTAMBULISHO WA VITO VYA TANZANIA





Na Wizara ya Madini

Katika kipindi ambacho mataifa yanajitahidi kujitambulisha kupitia ubora wa rasilimali na ubunifu wao, Tanzania imechukua hatua ya kimkakati ya kuitangaza dunia utajiri wake wa madini ya vito.

Kupitia Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) sasa yanageuka kuwa majukwaa muhimu ya kimataifa ya kuitambulisha Tanzania kupitia vito vyake adimu.

Kupitia uanzishwaji wa maduka ya kisasa ya vito vilivyoongezwa thamani katika maeneo hayo, TGC imefanikiwa kuunda zaidi ya sehemu za biashara. Maduka hayo yamekuwa majukwaa ya kimkakati ya kusimulia hadithi ya Tanzania, ambapo wageni wanafahamu historia, ubora na upekee wa madini ya vito yanayopatikana nchini.

Maduka hayo yamewekwa katika maeneo yanayopokea maelfu ya wageni wa ndani na wa kimataifa kila mwaka, wakiwemo watalii, wawekezaji, wasafiri na wajumbe wa mikutano ya kimataifa. Kupitia vituo hivyo, wageni hupata fursa ya kujifunza safari ya madini ya vito ya Tanzania kuanzia uchimbaji wake ardhini, kupitia elimu na teknolojia ya jemolojia, hadi kufikia bidhaa za mwisho zenye ubunifu na ubora wa viwango vya kimataifa.

Kwa sasa, wageni wanaowasili kupitia AICC na KIA wanaweza kununua vito halisi vya Tanzania kama tanzanite na aina nyingine za madini ya vito tayari vikiwa vimeongezewa thamani, badala ya kuuza malighafi pekee. Hatua hii inaongeza thamani ya rasilimali za taifa na kuifanya Tanzania kujitangaza duniani kupitia bidhaa zake za ubunifu.

Akizungumzia dhamira ya mpango huo, Mratibu wa TGC, Mhandisi Ally Maganga amesema uanzishwaji wa maduka hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa taifa wa kutumia sekta ya madini kuimarisha uchumi na diplomasia ya kiuchumi.

Amesema maduka hayo yanatoa fursa kwa wageni kukutana moja kwa moja na utambulisho wa Tanzania kupitia bidhaa zenye ubunifu wa Watanzania na utaalamu wa kitaaluma katika sekta ya vito.

Kwa upande wa utekelezaji wa kila siku, mwitikio wa wateja unaonesha mafanikio ya mpango huo. Edward, mmoja wa wauzaji katika maduka ya TGC, amesema wageni wengi huvutiwa kwanza na muonekano wa vito kabla ya kufurahishwa zaidi na simulizi ya asili na namna vilivyotengenezwa.

Amesema wageni wengi hununua vito hivyo kama kumbukumbu ya safari yao nchini au kama zawadi maalum kwa ndugu na marafiki, jambo linaloifanya Tanzania kuendelea kukumbukwa kimataifa.

Wageni kutoka Ulaya, Asia, Amerika na mataifa mbalimbali ya Afrika wameeleza kuvutiwa na ubora wa vito pamoja na maelezo ya kitaalamu wanayopewa kuhusu chanzo, aina na thamani ya kila kito. Uzoefu huo unaongeza uaminifu kwa bidhaa za Tanzania na kuimarisha taswira ya nchi kama kitovu cha vito adimu duniani.

Kupitia mpango huu, TGC inaendelea kujidhihirisha kama taasisi muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa uongezaji thamani wa madini ya vito. Pamoja na hilo, juhudi hizi zinachangia pia kuimarisha ajira kwa vijana waliobobea katika jemolojia, ubunifu wa vito na huduma za kitaalamu.

Kwa hakika, maduka ya TGC yaliyopo AICC na KIA yamekuwa zaidi ya vituo vya biashara. Yamegeuka kuwa maeneo ya simulizi ya taifa ambapo kila kito kinakuwa hadithi ya Tanzania, na kila mnunuzi anakuwa balozi wa kuitangaza nchi duniani.

Umuhimu wa Vijana wa Kitanzania katika Uongezaji Thamani wa Madini ya Vito

Katika safari ya Tanzania ya kujenga tasnia imara ya madini ya vito, vijana wa Kitanzania wameendelea kuwa nguvu kazi muhimu katika uongezaji thamani wa rasilimali hizo. Ushiriki wao katika ukataji, ung’arishaji, ubunifu wa vito, tathmini ya thamani na masoko unaifanya sekta hiyo kuwa ya kisasa, yenye tija na inayotoa ajira zenye ujuzi.

Kupitia TGC, vijana wanapata mafunzo ya kitaalamu katika taaluma za jemolojia, ubunifu wa vito, tathmini na uthibitishaji wa ubora kwa viwango vinavyotambulika kimataifa. Mafunzo hayo yanawawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa madini ya vito badala ya kubaki watazamaji wa rasilimali zao.

Hatua hiyo inaifanya rasilimali ya madini kubadilika kutoka kuwa urithi wa kijiolojia pekee na kuwa mtaji wa maarifa, ajira na fursa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Uimarishaji wa Mafunzo na Uhaulishaji wa Teknolojia Kupitia Ushirikiano wa Kimataifa

Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuimarisha ubora wa mafunzo ya wataalamu wazawa kwa kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) na Kampuni ya Sunset Gem kutoka Thailand.

Ushirikiano huo unalenga kuhamisha teknolojia na utaalamu wa kimataifa katika ukataji, ung’arishaji na utambuzi wa madini ya vito, pamoja na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma ili kuinua viwango vya mafunzo nchini.

Aidha, juhudi za Serikali za kujenga jengo la kisasa la ghorofa nane jijini Arusha kwa ajili ya TGC zinaonesha dhamira ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha kikanda cha elimu, biashara na ubunifu wa madini ya vito. Hatua hiyo pia inalenga kuwawezesha vijana wa Kitanzania kuwa wahusika wakuu wa tasnia ya vito katika soko la ndani na la kimataifa.










Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.