SAUTI ZA FILAMU YAANZA SAFARI YA KUWAFIKIA WASANII WA FILAMU TANZANIA BARA NA ZANZIBAR



Dar es Salaam,

Wakati tasnia ya filamu nchini ikiendelea kukua na kupiga hatua mpya, jukwaa la burudani na habari za filamu Sauti za Filamu limeanza mpango maalum wa kuwafikia wasanii wa filamu na michezo ya kuigiza kote nchini, kuanzia Tanzania Bara hadi visiwani Zanzibar.

Mpango huo unalenga kuibua na kuonesha vipaji vya waigizaji, watayarishaji, waongozaji pamoja na vikundi vya sanaa ambavyo mara nyingi hufanya kazi kubwa lakini hukosa nafasi ya kutambulika kwa upana katika jamii.

Kupitia hatua hiyo, jukwaa la Sauti za Filamu linakusudia kuifanya tasnia ya filamu kuwa karibu zaidi na wapenzi wa sanaa, huku likiwapa wasanii nafasi ya kuonekana na kusikika katika majukwaa ya kitaalamu.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Mwakilishi wa Sauti za Filamu Charles Mkoka amesema kwa muda mrefu wasanii wengi wamekuwa wakitegemea mitandao ya kijamii kujitangaza kupitia hashtags, ushirikiano wa kazi (collaborations) pamoja na algorithimu za majukwaa ya kidijitali, jambo ambalo wakati mwingine halitoshi kuwafikia wadau wengi wa tasnia.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukitegemea sana wasanii kunyanyuana kupitia hashtags, collaborations au hata algorithm za mitandao ya kijamii. Lakini ukweli ni kwamba hilo pekee halitoshi. Ndiyo maana Sauti za Filamu tumeamua kuwafikia wasanii moja kwa moja na kuhakikisha kazi zao zinaonekana na kusikika kwa wakati,” amesema Mkoka.

Ameeleza kuwa lengo kuu la jukwaa hilo ni kuhakikisha kila msanii awe maarufu au anayechipukia, wa mitandaoni au wa mtaani anapata nafasi ya kuonesha kazi zake na kuongeza wigo wa kufahamika ndani na nje ya Tanzania.

Katika miaka ya hivi karibuni, tasnia ya filamu nchini imeendelea kuzalisha filamu na tamthilia nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Hata hivyo, upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu kazi hizo bado ni changamoto kwa baadhi ya wadau na wapenzi wa sanaa, licha ya kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii.

Kupitia Sauti za Filamu, wapenzi wa sanaa wataweza kupata taarifa mbalimbali ikiwemo habari za filamu mpya, mahojiano ya wasanii, uchambuzi wa tasnia, taarifa za tuzo na matamasha pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya filamu.

Kwa sasa jukwaa hilo linaendelea kuwasiliana na wadau wa filamu kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram, Facebook, Threads na WhatsApp Channel kupitia akaunti ya @sautizafilamu, huku tovuti rasmi ya www.sautizafilamu.co.tz ikiwa kitovu kikuu cha habari na makala za tasnia ya filamu mtandaoni.

Aidha, maandalizi yanaendelea ya kufungua akaunti rasmi za TikTok na YouTube ili kuongeza wigo wa kuwafikia wapenzi wa filamu na burudani ndani na nje ya Tanzania.

Kwa mujibu wa waendeshaji wa jukwaa hilo, mipango ya Sauti za Filamu ni ya muda mrefu na inalenga kuwa sehemu ya mchango chanya katika kukuza na kuendeleza tasnia ya filamu nchini.

“Tunatamani kuona sanaa ya filamu inakua na kufikia hadhi inayostahili. Ndiyo maana tunalenga kuwasaidia hasa wasanii wachanga na wanaochipukia kupata jukwaa la kuonesha vipaji vyao na kufikia ndoto zao bila vikwazo vingi,” amesema mwakilishi wa Sauti za Filamu, ndugu Charles.


Kwa sasa wasanii, vikundi vya sanaa pamoja na makampuni ya filamu wanakaribishwa kutuma kazi zao ili ziweze kutangazwa na kupata nafasi ya kufahamika kupitia jukwaa hilo.

Kazi zinaweza kutumwa kupitia barua pepe sautizafilamu@gmail.com, ili kupata nafasi ya kuonekana kwenye jukwaa hilo ambalo linaendelea kujijengea nafasi kama moja ya majukwaa muhimu ya habari za tasnia ya filamu nchini.

Kwa habari zaidi, mahojiano ya kipekee ya wasanii pamoja na taarifa za filamu mpya, tembelea www.sautizafilamu.co.tz na ufuatilie Sauti za Filamu katika mitandao yake ya kijamii.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.