Arusha.
Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekamilisha ujenzi wa barabara ya Eso–Longdon yenye urefu wa kilomita 1.8 kwa kiwango cha lami katika Jiji la Arusha.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa na TARURA, Meneja wa TARURA katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Mhandisi Godfrey Bwire amesema barabara hiyo imekamilika na kazi iliyobaki ni uwekaji wa taa za barabarani pamoja na matuta.
“Katika mwaka huu wa fedha, serikali kupitia TARURA imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa barabara ya Eso–Longdon kwa kiwango cha lami. Kilichobaki ni uwekaji wa taa za barabarani na matuta,” amesema.
Amesema barabara hiyo imejengwa kwa kutumia mapato ya ndani na ina umuhimu mkubwa katika kupunguza msongamano wa magari, hasa katika eneo la soko la Kilombero linalojengwa kupitia mradi wa TACTIC.
Amefafanua kuwa barabara hiyo itatumika kama njia mbadala kwa watumiaji wa barabara wanaotoka Mromboo badala ya kuzunguka eneo la Sombetini, hivyo kusaidia kurahisisha usafiri na kupunguza msongamano.
Aidha, amesema utekelezaji wa miradi ya TACTIC unaendelea katika mwaka wa fedha 2025/2026, ikihusisha ujenzi wa kilomita 10.2 za barabara kwa kiwango cha lami.
Amezitaja barabara hizo kuwa ni pamoja na barabara ya Shelatoni yenye urefu wa kilomita 4.8, barabara ya Orasiti kilomita 3.96 na barabara inayoelekea Orjoro yenye urefu wa kilomita 1.475 ambako kunajengwa kituo kikubwa cha mabasi jijini Arusha.
Amesema miradi hiyo inalenga kuboresha usafiri, kupunguza msongamano wa magari na kuchochea shughuli za kiuchumi katika jiji hilo.
Pia Jiji la Arusha linaendelea kutekeleza miradi mingine kupitia TACTIC ikiwemo ujenzi wa stendi ya mabasi, masoko ya Kilombero na Moromboo pamoja na uboreshaji wa bustani ya Themi miradi hiyo ina thamani ya bilioni 30.6.
Mbali na miradi hiyo, amesema kuna miradi mingine inayotekelezwa kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara (Road Fund), ikiwemo ujenzi wa barabara kutoka Vijenge Juu hadi Ngurero, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Arusha.
Amesema mipango inaendelea ya kujenga barabara nyingine kwa kiwango cha lami ikiwemo barabara ya Kibo yenye urefu wa kilomita 3.55 kutoka Mromboo hadi Arusha Girls kupitia Uwanja wa Ndege, pamoja na barabara ya Lemala yenye urefu wa kilomita 4 kuelekea TBL na UNGA Limited.
Akizungumzia mwitikio wa wananchi, Mhandisi Bwire amesema wamepokea kwa furaha ujenzi wa barabara hizo kwani hapo awali zilikuwa na changamoto kubwa hasa wakati wa mvua na vumbi wakati wa kiangazi.
Amewataka wananchi kutunza miundombinu hiyo kwa kuepuka kutupa taka katika mitaro ya maji na kuhakikisha inasafishwa mara kwa mara ili kuruhusu maji kupita vizuri.
Pia amewahimiza kulinda taa za barabarani ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na kusaidia kuimarisha usalama wakati wa usiku.
Amesema serikali hutumia gharama kubwa kujenga miundombinu hiyo hivyo ni wajibu wa wananchi kuilinda na kuitunza kwa manufaa ya wote.



Hakuna maoni: