SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA MIZANI ZA KIDIGITALI KUONDOA UDANGANYIFU WA MAZAO

Dodoma

Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imezitaka Vyama vya Ushirika wa Mazao nchini kutumia mizani za kidigitali katika upimaji wa mazao ili kuondoa udanganyifu na kuhakikisha wakulima wanapata haki zao.

Wito huo umetolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, ambaye amesema matumizi ya mizani hizo yatasaidia kuongeza uwazi katika biashara ya mazao na kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi za uzalishaji na mauzo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maelekezo hayo yalitolewa kupitia barua ya Machi 13, 2026 kwa wenyeviti na wajumbe wa bodi za vyama vya ushirika wa mazao Tanzania Bara, akisisitiza umuhimu wa kutumia mizani za kidigitali kwa lengo la kulinda maslahi ya wakulima.

Dkt. Ndiege ameonya kuwa vyama vitakavyoshindwa kuwa na mizani hizo au kutumia kinyume na malengo yaliyokusudiwa vitachukuliwa hatua za kisheria. Aidha, wakulima wametakiwa kuhakikisha mazao yao yanapimwa kwa kutumia mizani zilizounganishwa na Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) ili kupata malipo sahihi.

Pia amevitaka vyama ambavyo bado havijatekeleza maelekezo ya ununuzi wa mizani hizo kuhakikisha vinazingatia taratibu zilizowekwa na kukamilisha zoezi hilo ifikapo Juni 31, 2026.

TCDC imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika nchini, ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo madhubuti ya ununuzi na matumizi sahihi ya mizani za kidigitali ili kuboresha sekta ya kilimo na masoko ya mazao.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.