STAMICO, PLANET ONE ZASAINI MKATABA WA KIHISTORIA UCHIMBAJI MADINI YA KINYWE MIRERANI

Mirerani, Simanjiro – Manyara

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ameshuhudia Utiaji Saini wa Mkataba wa uendelezaji wa leseni za utafiti wa madini ya Kinywe (Graphite) kati ya Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya Planet One Natural Resources Holdings PTE LTD ya Singapore.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kiruswa amesema mkataba huo ni hatua muhimu itakayochochea maendeleo endelevu katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro na Mkoa wa Manyara kwa ujumla.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo unapaswa kuwanufaisha wananchi wa eneo husika kwa kuwapa kipaumbele katika ajira pamoja na kushirikishwa kikamilifu katika shughuli za kiuchumi zinazotokana na mradi huo.

“Ni muhimu kuhakikisha wafanyakazi wanatoka Mirerani na maeneo ya jirani, lakini pia kampuni zinunue bidhaa na huduma kutoka Simanjiro ili kuongeza mzunguko wa fedha kwa wananchi,” amesema Dkt. Kiruswa.

Aidha, amesema madini ya Kinywe ni madini mkakati yenye mahitaji makubwa duniani, hususan katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme, hivyo kutoa fursa adhimu kwa Tanzania kiuchumi.

Katika hatua nyingine, amezitaka STAMICO pamoja na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuendelea kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapatia taarifa sahihi za kijiolojia ili kuongeza tija katika shughuli zao.

Dkt. Kiruswa amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya sekta ya madini kuwa kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, amesema shirika hilo linaendelea kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini, huku akibainisha kuwa huu ni mkataba wa tatu kusainiwa ndani ya mwaka huu.

“Hii inaonesha wazi kuwa Tanzania imeendelea kuwa kivutio cha uwekezaji katika sekta ya madini. Mradi huu utazalisha ajira nyingi, hususan kwa wananchi wa Mirerani,” amesema Dkt. Mwasse.

Ameongeza kuwa mradi huo utachangia kuongeza mapato ya Serikali kupitia fursa mbalimbali zitakazotokana na shughuli zake.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Balozi Simon Sirro, amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia rasilimali za madini.

Amewataka wananchi wa Simanjiro kushirikiana na wawekezaji pamoja na kuzingatia uadilifu, hasa kwa wale watakaopata fursa za ajira katika mradi huo.

Kwa mujibu wa Balozi Sirro, mapato ya STAMICO yameongezeka kutoka shilingi bilioni 19.81 mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia shilingi bilioni 72.99 mwaka 2024/25, jambo linaloashiria ukuaji wa shirika hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Planet One Natural Resources Holdings PTE LTD, Bw. Ramakrishna Chinnamsetty, amesema mkataba huo utaimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Singapore.

“Mradi huu ni zaidi ya uchimbaji wa graphite; utachochea maendeleo ya miundombinu, afya, elimu na teknolojia. Tumejipanga kuheshimu mazingira, utamaduni na kushirikiana na jamii,” amesema Chinnamsetty. 

Ameongeza kuwa mradi huo utaisaidia Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa madini ya Kinywe duniani.

“Leo tumepanda mbegu ya pamoja ambayo itakua na kuleta manufaa kwa pande zote,” ameongeza Chinnamsetty.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amesema Wizara inaendelea kusimamia sekta hiyo kwa kuzingatia Sera, Sheria na mifumo madhubuti ya kuendeleza utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani wa madini nchini. 

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.