TPBRC KUANDAA “BOXING MEDIA DAY” KUINUA TASNIA YA NGUMI NCHINI


Na Mwandishi Wetu

Chama cha Makocha wa Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kinatarajia kuandaa siku maalum ya Boxing Media Day itakayofanyika Aprili 15, mwaka huu, kwa kutembelea kambi mbalimbali za mazoezi ya ngumi (gym).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Machi 30, 2026, Mwenyekiti wa chama hicho, Jaffary Ndame, amesema kuwa tukio hilo linalenga kuonesha na kutangaza kazi zinazofanywa na makocha wa ngumi pamoja na shughuli za chama kwa ujumla.

Ndame alifafanua kuwa TPBRC ina dhamira ya kuwa chachu ya maendeleo ya mchezo wa ngumi nchini kwa kuinua taaluma ya ukocha na kukuza vipaji vya mabondia watakaoiwakilisha vyema Tanzania kimataifa.

 “Sisi walimu wa ngumi za kulipwa tunatarajia kuona matunda makubwa ya kazi yetu ya kuwanoa mabondia na kuendeleza mchezo huu,” amesema Ndame.

Kwa upande wake, Katibu wa chama hicho, Jumma Mbogo, ametaja kamati zitakazohusika kufanikisha tukio hilo kuwa ni pamoja na kamati ya ufundi, nidhamu, afya, pamoja na habari na mawasiliano.

Mbogo pia amesema kuwa Boxing Media Day imedhaminiwa na Robby Farmer’s, huku akitoa wito kwa wadau na wadhamini wengine kujitokeza ili kuunga mkono jitihada za kukuza sekta ya ngumi za kulipwa nchini.

Naye Mweka Hazina wa chama hicho, Hamis Richard, amesema TPBRC itaweka mkazo katika kuhakikisha makocha wananufaika na mikataba yenye tija ili kuboresha maisha yao na kuwaondoa katika changamoto za kiuchumi.

Kwa upande wa Meneja wa Habari na Mawasiliano, Somba Dauka, amesema wadhamini hao wameandaa zawadi maalum kwa mabondia wanawake wanaofundishwa na makocha wanawake katika kumbi mbalimbali za mazoezi.

Dauka aliongeza kuwa chama hicho pia kina mpango wa kuimarisha na kuongeza muda wa mapambano ya ngumi kwa wanawake, tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo yalifanyika kwa muda mfupi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.