DAR ES SALAAM.
Katika kuendeleza dhamira ya uwajibikaji kwa jamii, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), tarehe 19 Machi 2026, lilifanya ziara ya kutembelea vituo vitatu vya watoto wenye mahitaji maalum jijini Dar es Salaam, na kutoa misaada mbalimbali kwa lengo la kuleta faraja na matumaini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji ,Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Bi. Irene Gowelle, alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kushirikiana na jamii kwa vitendo kwa kutoa misaada hususan kwa makundi ya watoto yenye uhitaji .
Alieleza kuwa msaada huo haujalenga tu kukidhi mahitaji ya msingi, bali pia kuwajengea watoto hao imani, matumaini na ujasiri wa kuendelea kuamini katika ndoto zao licha ya changamoto wanazokabiliana nazo.
“Leo TANESCO tumeshiriki na watoto hawa wenye mahitaji maalum kwa kutoa misaada mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kurejesha kwa jamii na kuendeleza uwajibikaji wetu wa kijamii,” alisema Bi. Irene.
Aidha, alisisitiza kuwa TANESCO itaendelea kushirikiana na jamii inayowazunguka kama sehemu ya mchango wake katika kujenga taifa lenye mshikamano, upendo na ustawi wa pamoja.
Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Kituo cha Umra Orphanage Center, Bi. Rahma Juma, aliipongeza TANESCO kwa hatua hiyo, akisema msaada uliotolewa umefika kwa wakati muafaka na umeleta faraja kubwa kwa watoto pamoja na walezi wao.
Alibainisha kuwa ujio wa TANESCO umeongeza furaha na kuwapa watoto motisha mpya, huku akieleza kuwa vituo vya aina hiyo bado vinakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji ushirikiano wa wadau.
“Kazi hii iliyofanywa na TANESCO ni mfano wa kuigwa. Msaada huu umekuja kwa wakati mwafaka na utatusaidia sana katika malezi ya watoto tulionao hapa kituoni,” alisema Bi. Rahma.
"Napenda kuwashukuru TANESCO kwa ujio wao kwetu tunashukuru kwa sadaka ambazo wameleta hasa katika msimu huu wa sikukuu zimekuja kwa wakati sahihi wametuletea vitu ambavyo ni mahitaji yetu ya kila siku " Amesema Bi. Nuru Mwegoha
Aidha, alitoa wito kwa taasisi, makampuni na watu binafsi kujitokeza kusaidia makundi yenye mahitaji maalum ili kuhakikisha wanapata huduma bora na kuishi maisha yenye matumaini.
Vituo vilivyofikiwa katika ziara hiyo ni Umra Orphanage Center kilichopo Magomeni, Kituo cha Watoto Yatima cha CHAKUWAMA kilichopo Sinza Mori, pamoja na New Hope for Girls Organization kilichopo Kimara.





Hakuna maoni: