PRETORIA.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe pamoja na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula wamewasili jijini Pretoria, Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 47 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika Machi 12 na 13, 2026.
Mawaziri hao waliwasili Machi 11, 2026 na kutembelea Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ambapo walipokea taarifa kutoka kwa wataalamu kuhusu majadiliano ya vikao vya utangulizi vilivyofanyika kabla ya mkutano huo.
Vikao hivyo ni pamoja na Kikao cha Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi kilichopitia utekelezaji wa Mpango Mkakati Elekezi wa Maendeleo wa Kanda (RISDP) kilichofanyika Machi 4 na 5, 2026; Kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu kilichofanyika Machi 7 na 8, 2026 pamoja na Kikao cha Kamati ya Fedha kilichofanyika Machi 9, 2026.
Aidha, Mawaziri hao walipokea taarifa kuhusu ushiriki wao katika Mkutano wa 47 wa Baraza la Mawaziri wa SADC utakaofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye majengo ya Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini jijini Pretoria.
Wakiwa katika ofisi za ubalozi huo, mawaziri hao pia walipokea taarifa kuhusu hali ya uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na eneo la uwakilishi iliyowasilishwa na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. James Bwana.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa aliongoza ujumbe wa Tanzania katika vikao vya utangulizi vilivyotangulia mkutano huo wa Baraza la Mawaziri wa SADC.





Hakuna maoni: