Dar es Salaam.
Waandishi wa habari wanawake wamepata mafunzo maalum kuhusu masuala ya mazingira katika warsha iliyofanyika Machi 11, 2026 jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Warsha hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Weka Mazingira Safi (WEMASA) imelenga kuwajengea uwezo wanahabari hao ili waweze kuelimisha jamii kwa ufanisi zaidi kuhusu changamoto za mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akiwasilisha mada katika warsha hiyo, mshauri wa masuala ya mazingira na mwakilishi wa taasisi ya Connect, Carlos Mdemu, aliwahimiza wanahabari kuendelea kuandika na kuripoti kwa kina masuala ya mazingira ili kusaidia jamii kuelewa madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira.Ameeleza kuwa tafiti zinaonyesha kila mtu huzalisha takribani kilo moja ya taka kwa siku, lakini nyingi ya taka hizo hazitupwi kwa njia sahihi hali inayochangia kuenea kwa magonjwa na uharibifu wa mazingira.
“Taka zinaweza kusababisha magonjwa mbalimbali, si kipindupindu pekee. Baadhi ya taka ni za kemikali, nyingine hutokana na bidhaa zinazooza na zipo ambazo haziozi kabisa,” alisema.
Hata hivyo, Mdemu alibainisha kuwa taka zinaweza pia kuwa chanzo cha ajira na kipato ikiwa zitatumika vizuri. Alitolea mfano taka za plastiki ambazo kwa sasa zinakusanywa na kuuzwa kwa ajili ya kuchakata, hatua inayosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira huku ikizalisha kipato.
Pia alieleza kuwa taka za vyakula kutoka masokoni zinaweza kutumika kutengeneza mbolea au kuzalisha wadudu funza wanaotumika kama chakula cha kuku na samaki.
Alisisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mtu na elimu kuhusu umuhimu wake inapaswa kuanzia katika familia, maeneo ya kazi na hata barabarani.Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, Jiji la Dar es Salaam huzalisha takribani tani 5,000 za taka kila siku. Kati ya hizo, asilimia 31 hutupwa ovyo, asilimia 23 huchomwa moto, asilimia 37 huzikwa ardhini, asilimia 1 huzagaa barabarani, huku asilimia 5 zikikusanywa na kutupwa katika maeneo rasmi na asilimia 3 kushughulikiwa kwa njia zisizo rasmi.
Baadhi ya wadhamini wa warsha hiyo, akiwemo Taifa Gas pamoja na UTT AMIS, walieleza umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kama njia ya kulinda afya za wananchi na mazingira.
Akizungumza katika warsha hiyo, Meneja wa Uhusiano na Masoko wa Taifa Gas, Oscar Shelukindo, alisema ni asilimia ndogo ya wananchi wanaotumia nishati safi, huku wengi wakiendelea kutegemea kuni na mkaa kwa shughuli za kupikia.
Alisema gharama za awali za kununua mitungi ya gesi pamoja na urahisi wa kupata nishati mbadala kama kuni na mkaa ni miongoni mwa sababu zinazochangia watu wengi kutotumia gesi ya kupikia.
Hata hivyo, alifafanua kuwa matumizi ya gesi yana faida nyingi ikiwemo kupika kwa haraka na kutoa moto wa uhakika zaidi ukilinganisha na kuni.
Aidha, alieleza kuwa Taifa Gas tayari imeanzisha kiwanda cha kutengeneza mitungi ya gesi mkoani Pwani ili kupunguza utegemezi wa kuagiza mitungi kutoka nje ya nchi.
Mwandishi mwandamizi aliyeshiriki warsha hiyo, Dina Ismail, alisema mafunzo hayo yameongeza uelewa wake kuhusu nafasi ya wanawake katika kulinda mazingira, hasa katika matumizi ya nishati safi majumbani.
Kwa ujumla, warsha hiyo imeonyesha umuhimu wa kushirikisha wanahabari wanawake katika kuhamasisha jamii kutunza mazingira na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.











Hakuna maoni: