DODOMA
AJIRA mpya 1,439 zinatarajiwa kutolewa katika sekta ya nishati huku watumishi 5,207 wakipatiwa mafunzo maalum ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na utoaji huduma kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi alipokuwa akiwasilisha mpango wa wizara yake bungeni jijini Dodoma ambapo alisema Serikali imejipanga kuimarisha rasilimaliwatu katika sekta hiyo muhimu.
Amesema mbali na ajira hizo mpya, pia watumishi 933 watapandishwa vyeo ikiwa ni sehemu ya kuongeza motisha na tija kazini, huku Wizara ikiendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Aidha, amebainisha kuwa mafunzo yatakayotolewa kwa watumishi yatakuwa ya muda mfupi na mrefu ndani na nje ya nchi, yakilenga kuwajengea uwezo katika nyanja mbalimbali ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sekta ya nishati.
Kwa upande wa ustawi wa watumishi, Ndejembi amesema Serikali itaendelea kutekeleza programu za kulinda afya na nguvu kazi ikiwemo kudhibiti magonjwa sugu, kuimarisha afya ya akili na kupambana na maambukizi ya VVU/UKIMWI pamoja na vita dhidi ya rushwa kwa kutumia mifumo ya TEHAMA.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Serikali itaendelea kushirikisha sekta binafsi katika miradi ya nishati kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo REA, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na EWURA ili kuongeza uwekezaji na upatikanaji wa nishati nchini.

Hakuna maoni: