BODABODA WAFANYABIASHARA NA WAJASIRIAMALI KIGAMBONI WALALAMIKIA KUFUKUZWA ENEO LA KAZI

 


Na Mwandishi Wetu

Wafanyabiashara, wajasiriamali pamoja na waendesha bodaboda katika Wilaya ya Kigamboni, eneo la Kibada Stand, wamelalamikia hatua ya kufukuzwa na kujengewa uzio katika eneo lao la kazi, wakidai hali hiyo inahatarisha kipato chao cha kila siku na ustawi wa biashara zao.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wafanyabiashara hao wakiwemo wamiliki wa maduka, wauza samaki na bidhaa mbalimbali wamesema wamekuwa wakisumbuliwa mara kwa mara na askari wa Halmashauri (migambo), ambao huvamia maeneo yao hasa nyakati za usiku na kuvunja meza pamoja na kuharibu bidhaa zao, jambo linalowasababishia hasara kubwa.

“Tumekuwa tukifanya biashara hapa kwa muda mrefu bila matatizo makubwa, lakini siku hizi hali imekuwa tofauti. Migambo wanakuja usiku, wanabomoa meza zetu, wanatupa bidhaa zetu na wakati mwingine wanachukua kabisa mizigo yetu,” amesema mmoja wa wafanyabiashara hao kwa masikitiko.

Akizungumza kwa niaba ya waendesha bodaboda, Mwenyekiti wa Kijiwe cha Kivumbi, amesema tayari walishafanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni ambaye aliwaruhusu kuendelea kufanya kazi katika eneo hilo, lakini bado baadhi ya viongozi wa chini wamekuwa wakikiuka maelekezo hayo.

“Tumekutana na Mkuu wa Wilaya, akatupa ruhusa tuendelee kufanya kazi hapa, lakini cha kushangaza viongozi wa chini wanakuja na kutufukuza kama vile hakuna maelekezo yaliyotolewa. Hii inatuchanganya sana na kutunyima haki yetu ya kufanya kazi,” amesema.

Waendesha bodaboda hao wameeleza kuwa kijiwe chao kimekuwepo kwa muda mrefu na kimekuwa sehemu muhimu ya huduma kwa wakazi wa eneo hilo, wakisisitiza kuwa kuhamishwa kwenda sokoni si suluhisho kutokana na kukosekana kwa wateja wa kutosha.

“Wanasema tuhame twende sokoni, lakini kule hakuna wateja wa kutosha. Hapa ndipo kuna mzunguko wa watu, hapa ndipo tunapata wateja wa kuwahudumia na kupata kipato cha kuendesha familia zetu,” amesema mmoja wa madereva wa bodaboda.

Kwa upande wao, wafanyabiashara wa maduka wamelalamikia uwekaji wa uzio unaodaiwa kujengwa mbele ya maduka yao kwa ajili ya bustani, wakisema unazuia wateja kuwafikia kwa urahisi na hivyo kupunguza mauzo.

“Huu uzio umewekwa mbele kabisa ya maduka yetu. Wateja wanapata tabu kupita, wengine wanaamua kuondoka kabisa. Hiki walichofanya si haki, wanapaswa kufikiria athari zake kwa sisi tunaotegemea biashara hizi,” amesema mmoja wa wauza duka.

Nao wafanyabiashara wa samaki wameeleza kuwa wamekuwa wakihimizwa kuhamia sokoni, lakini mazingira ya soko hilo hayalingani na muda wao wa biashara, kwani wao hufanya kazi hadi usiku wa manane huku soko likifungwa mapema.

“Sisi hatujakataa kwenda sokoni, lakini changamoto ni muda. Soko linafungwa mapema, sisi tunafanya kazi mpaka usiku. Tukija huku tunafukuzwa na migambo. Tumekopa mitaji, tunatafuta marejesho, sasa kwa hali hii tutafanikiwa kweli?” amehoji mmoja wao.

Wafanyabiashara hao wameongeza kuwa wengi wao wamechukua mikopo kwa ajili ya kuendesha biashara zao, hivyo hali ya kufukuzwa mara kwa mara inawaweka katika hatari ya kushindwa kurejesha mikopo hiyo.

“Tunamwomba mama yetu, Rais Samia Suluhu Hassan, atusikie. Ametuwezesha kupata mikopo kwa nia njema, lakini kwa hali hii ya kufukuzwa na kubugudhiwa, tutashindwa kabisa kurejesha mikopo hiyo,” wamesema kwa pamoja.

Aidha, wametoa wito kwa uongozi wa Wilaya ya Kigamboni na Halmashauri husika kukaa nao mezani na kutafuta suluhisho la kudumu litakalowezesha wao kuendelea na shughuli zao bila bughudha, huku wakizingatia pia taratibu za mji na mipango ya maendeleo.

“Tunachohitaji si ugomvi, tunahitaji suluhisho. Tuko tayari kushirikiana na serikali, lakini tunataka mazingira rafiki ya kufanya kazi kwa amani,” wamehitimisha.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.