EACOP YAWEKA REKODI YA SAA MILIONI 6 BILA AJALI KAZINI

Na Mwandishi Wetu, 

Tanga.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umeendelea kuonesha dhamira yake ya kulinda maisha ya wafanyakazi baada ya kufikia zaidi ya saa milioni sita za kazi bila kurekodi ajali yoyote kazini.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi yaliyofanyika Chongoleani mkoani Tanga, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa EACOP, Paul Hiegel, alisema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji thabiti wa kauli mbiu ya “Zero Harm” (Hakuna Madhara Sehemu ya Kazi).

Alisema mradi huo umeweka usalama kuwa kipaumbele cha kwanza kwa kuhakikisha kila mfanyakazi anatekeleza majukumu yake katika mazingira salama.
“Tunajivunia kuona wafanyakazi wetu wanarudi nyumbani salama na kuungana na familia zao wakiwa na furaha,” alisema.

Aliongeza kuwa usalama si tukio la siku moja bali ni utamaduni unaojengwa kila siku. Kupitia kauli mbiu ya mwaka huu, “Mind on Target, Eyes on Target,” EACOP inalenga kuongeza umakini wa wafanyakazi katika kutambua na kuepuka hatari.
“Tunataka kila mfanyakazi arejee nyumbani akiwa salama, bila majeraha yoyote,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka wafanyakazi kuzingatia matumizi ya vifaa vya kujikinga (PPE) muda wote wanapokuwa kazini, akieleza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kujilinda na kulinda wengine.

Kwa upande wake, Mkuu Msaidizi wa Kambi ya MTT (Marine Tanks Terminal), Jerome Betat, alisema mradi huo unahusisha wafanyakazi kutoka mataifa mbalimbali, hivyo usalama wao ni jambo la msingi hadi wanaporejea salama nyumbani baada ya kukamilika kwa mradi.

Alibainisha kuwa EACOP imewekeza katika mafunzo ya mara kwa mara pamoja na mifumo madhubuti ya usalama ili kupunguza hatari kazini.

Naye Meneja wa Usalama wa Afya na Mazingira, Stay Bidgewater, alisema maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kuwakumbusha wafanyakazi wajibu wao katika kudumisha usalama, akibainisha kuwa huu ni mwaka wa tano kwa mradi huo kuadhimisha siku hiyo tangu ulipoanza.

Alisema wafanyakazi wanaruhusiwa kusimamisha kazi mara moja wanapoona hatari yoyote bila kusubiri ruhusa kutoka kwa wasimamizi.
“Lengo ni kuzuia ajali kabla hazijatokea,” alisema.

Aliongeza kuwa kupitia kampeni ya “Zero Harm,” mradi huo hutoa zawadi kila mwezi kwa wafanyakazi wanaochangia kuzuia ajali, hatua inayosaidia kupunguza gharama za matibabu na kuongeza ufanisi kazini.

Mwakilishi wa EWURA, Salum Inegeja, aliipongeza EACOP kwa juhudi zake za kuhakikisha wafanyakazi wanazingatia matumizi ya vifaa vya kujikinga kama inavyotakiwa kisheria.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa EACOP, Catherine Mbatia, alisema maadhimisho hayo yanaonesha dhamira ya mradi huo katika kuweka usalama mbele.
“Lengo ni kuhakikisha kila mfanyakazi anakuja kazini salama na kurejea nyumbani salama,” alisema.

Aliongeza kuwa wafanyakazi wanahimizwa kutoa taarifa za hatari mapema, huku kila siku kabla ya kuanza kazi wakifanya tathmini ya shughuli za siku iliyopita ili kuboresha usalama zaidi.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo ya uendeshaji mitambo, Sifa Obadia, alisema mafunzo hayo yameongeza uelewa wa wafanyakazi kuhusu umuhimu wa usalama kazini.
“Tunazingatia usalama ili kuhakikisha hakuna madhara kwa watu wala miundombinu,” alisema.

Mradi wa EACOP unamilikiwa na TotalEnergies kwa asilimia 62, huku TPDC na UNOC kila moja likimiliki asilimia 15, na CNOOC ikimiliki asilimia 8.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.