KAMPENI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YAWAFIKIA WACHOMAJI WA NYAMA MSALATO, DODOMA

Na Mwandishi Wetu,

Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) imeendelea na kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wachomaji nyama katika maeneo mbalimbali jijini Dodoma.

Kampeni hiyo iliyoanzia mnada wa Msalato imelenga kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara hao kuhusu umuhimu wa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia nishati safi na endelevu.

Akizungumza wakati wa kampeni hiyo, Mtaalamu wa masuala ya nishati safi ya kupikia kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Mjiolojia Bw. Deo Alex, alitoa elimu kwa wachomaji nyama kuhusu faida za kutumia nishati safi kama gesi na majiko banifu, akibainisha kuwa teknolojia hizo ni rafiki kwa mazingira na zinaongeza ufanisi katika shughuli za uchomaji nyama.

Alieleza kuwa matumizi ya nishati safi huchangia kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti holela, pamoja na kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi wa kuni na mkaa, hususan magonjwa ya mfumo wa upumuaji.

Aidha, Bw. Alex alisisitiza kuwa serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi, hususan wajasiriamali wadogo, kuhamia kwenye matumizi hayo endelevu.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa nyama choma katika eneo hilo, Masumbuko Daudi, alisema kuwa elimu hiyo imewasaidia kuelewa kwa undani faida za nishati safi, akibainisha kuwa licha ya changamoto za gharama za awali, wako tayari kuanza mabadiliko hayo kwa manufaa ya afya na biashara zao.

Aidha, wananchi na wafanyabiashara wengine walioshiriki katika kampeni hiyo waliipongeza Wizara ya Nishati na UNCDF kwa kutoa elimu hiyo, wakisema itaongeza uelewa na kuchochea mabadiliko chanya katika matumizi ya nishati safi nchini.

Kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali na wadau wake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, ikiwa ni mkakati wa kulinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.