Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kimeadhimisha siku ya jinsia ya chuo (CBE Gender Day) ikiwa ni sehemu ya kuendeleza ajenda ya usawa wa kijinsia, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Maadhimisho hayo yameongozwa na Mgeni Rasmi, Bi Fatuma Abdallah Mkurugenzi Mtendaji wa Energy’s, ambaye amesisitiza kuwa usawa wa kijinsia si suala la maadhimisho pekee bali ni msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi, ubora wa maamuzi na ufanisi wa taasisi.
Ameipongeza CBE kwa kuendelea kuimarisha usawa wa kijinsia kupitia sera na utekelezaji wake, huku akibainisha kuwa licha ya jitihada hizo bado wanawake wanakumbana na changamoto mbalimbali katika sehemu za kazi, ikiwemo vitendo vya ukatili na ukosefu wa fursa sawa.
Ameongeza kuwa tangu ajiunge na shirika hilo mwaka 2023, wanawake walikuwa ni asilimia sita pekee, lakini kwa sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia asilimia 27, hatua inayodhihirisha dhamira ya dhati ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya nishati.
Pamoja na hayo Bi. Fatuma amesema Puma na CBE wanaushirikiano wa karibu unalenga kuimarisha usawa wa kijinsia pamoja na kuongeza ujuzi na weledi kwa wanafunzi, hususani katika sekta ya nishati.
Amesema chuo kimezindua mpango wa jinsia wa muda mrefu unaolenga kuendeleza mafanikio ya usawa wa kijinsia kwa zaidi ya miaka 50 tangu kuanza kwa jitihada hizo, huku kikihakikisha wanawake na wanaume wanapata fursa sawa katika elimu na maendeleo ya kitaaluma.
Pia ameeleza kuwa chuo kimeanza programu ya “double degree” inayowawezesha wanafunzi kusoma kwa miaka miwili nchini na kisha kwenda kukamilisha mwaka mmoja nchini China, hatua inayowaandaa zaidi kwa ushindani wa kimataifa.






Hakuna maoni: