Na Mwandishi Wetu,
Tabora.
Maafisa na askari 39 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Magharibi wamevalishwa vyeo, hatua inayolenga kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika uhifadhi wa rasilimali misitu nchini.
Akizungumza katika hafla ya uvalishaji vyeo iliyofanyika leo Aprili 23, 2026 katika ofisi za TFS Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi na Meneja wa Utawala, SACC. Erasto Luoga, aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi TFS, alisema kupandishwa kwa maafisa hao ni ishara ya kuongezewa mamlaka, wajibu na imani kutoka Serikalini.
Alisisitiza kuwa ni wajibu kwa Maafisa na Askari waliovalishwa vyeo kuonesha weledi wa hali ya juu, uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao, hasa katika kulinda na kusimamia rasilimali misitu ambazo ni mhimili muhimu wa uchumi na mazingira ya Taifa.
“Vyeo hivi viwe chachu ya kuongeza bidii, nidhamu na ufanisi kazini. Tunatarajia kuona matokeo chanya katika usimamizi na ulinzi wa misitu,” alisema SACC. Luoga.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Jackson Msaki, alisema hatua hiyo inaakisi imani kubwa ya Serikali kwa watumishi hao, hivyo wanapaswa kuitendea haki kwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Aliongeza kuwa nidhamu, uzalendo na uwajibikaji vitakuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha taasisi hizo zinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Hafla hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuimarisha taasisi zake za uhifadhi kwa kuwajengea uwezo watumishi wake na kuongeza motisha katika utendaji kazi wa kila siku.





Hakuna maoni: