MAENDELEO BANK YAENDELEA KUNG'ARA SOKONI, YAPATA FAIDA KWA MIAKA 11 MFULULIZO

Na Mwandishi Wetu,

Dar es Salaam. 

Benki ya Maendeleo Bank PLC imeendelea kuonesha uimara wa kifedha baada ya kurekodi ongezeko la faida kwa miaka 11 mfululizo tangu mwaka 2015, hatua inayoakisi ukuaji thabiti wa biashara na kuimarika kwa imani ya wateja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Fedha wa benki hiyo, Nolasco Charles amesema mafanikio hayo yanatokana na uongozi wenye maono pamoja na utekelezaji madhubuti wa mikakati ya kibiashara.

Amebainisha kuwa mwaka ulioishia Desemba 31, 2025, benki imepata mapato ya jumla ya shilingi bilioni 29.05 kutoka bilioni 23.00 mwaka 2024, sawa na ukuaji wa asilimia 26.

Aidha, mapato halisi yatokanayo na riba yaliongezeka hadi shilingi bilioni 25.78 kutoka bilioni 20.06, huku faida kabla ya kodi ikifikia shilingi bilioni 5.02 kutoka bilioni 3.85, sawa na ukuaji wa asilimia 30. Faida baada ya kodi nayo iliongezeka hadi shilingi bilioni 4.75 kutoka bilioni 3.68.

Kwa mujibu wa Charles, ukuaji huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuimarika kwa utoaji wa mikopo pamoja na kuongezeka kwa amana za wateja, zilizokua kwa asilimia 31 hadi kufikia shilingi bilioni 136.20 mwaka 2025.

“Ubora wa mikopo umeendelea kuimarika, ambapo mikopo chechefu imepungua hadi asilimia 4.51 kutoka asilimia 4.76 mwaka uliotangulia,” amesema  

Katika hatua nyingine, amebainisha kuwa thamani ya hisa za benki hiyo katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 600, kutoka shilingi 38 mwezi Aprili 2025 hadi shilingi 2,480 Aprili 13, 2026, jambo linaloonesha imani kubwa ya wawekezaji.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka sita wa 2025–2030 unaolenga kuimarisha rasilimali watu, kuendeleza teknolojia na kupanua huduma za kidigitali ikiwemo mobile banking na internet banking.

Hata hivyo, benki hiyo imeeleza kuendelea kuweka mkazo katika usimamizi wa vihatarishi ili kuhakikisha ukuaji wake unakuwa endelevu na salama.

Kuhusu mwaka 2026, Charles amesema benki imejipanga kupanua zaidi biashara huku ikiweka kipaumbele kwa wateja kwa kutoa huduma bunifu na rahisi zitakazokidhi mahitaji yao.

Aidha amewashukuru wafanyakazi wa benki hiyo pamoja na wateja kwa ushirikiano wao, akisema mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya juhudi za pamoja.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.