DC MKUDE AKABIDHI VYOMBO VYA USAFIRI TANESCO MKOA WA ARUSHA KUIMARISHA UTOAJI HUDUMA




Na Mwandishi Wetu, 
Arusha.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mkoani Arusha Mhe. Joseph Mkude amekabidhi vitendea kazi vya usafiri kwa TANESCO Mkoa wa Arusha ili kuimarisha utoaji wa huduma mbalimbali za Shirika kwa wananchi. 

Akizungumza tarehe 13, Aprili 2026 wakati wa hafla ya kukakabidhi vitendea kazi hivyo iliyofanyika katika Ofisi za TANESCO Mkoa wa Arusha amesema hatua hiyo ya kukabidhi vitendea kazi hivyo ni hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za umeme wa uhakika bila vikwazo vyoyote.

Amesema vitendea kazi hivyo vinakwenda kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa watumishi wa TANESCO katika wilaya za Mkoa wa Arusha na kuwawezesha kutatua changamoto za wateja kwa wakati kwani Magari pamoja na Bajaji zitawawezesha kuyafikia maeno mengi zaidi ili kufikisha huduma ya umeme.

Amewataka Watumishi wa TANESCO Mkoa wa Arusha kuhakikisha wanatumia vyema vitendea kazi hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa na Shirika na wala sio kwa matumizi yao binafisi ambayo hayana faida wala mchango wowote kwa Shirika hasa katika kutoa huduma kwa wananchi.

“Haya Magari tuliyopatiwa katika Mkoa wetu yanakwenda kugawiwa katika kila wilaya naomba yakatumike ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa, tusitumie Magari haya kwa mambo yetu binafsi yasiyo na tija katika kutoa huduma kwa wananchi”.

Kwa upande wake Meneja wa Huduma za Usalama TANESCO Bw. Lenin Kiobya amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iliwezesha kununuliwa kwa Magari Makubwa na Madogo zaidi ya 500 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Bw. Kiobya amesema kati ya Magari hayo zaidi ya 500, Malori ya ukubwa mbalimbali ikiwemo tani 10 na tani 7 yapo 215 ambayo yanakwenda kuwa msaada Mkubwa zaidi katika huduma za matengenezo ya umeme kwa wakati hali itakayochangia kuongeza ufanisi wa kazi ndani ya Shirika.

Aidha, amesema kwa Mwaka wa Fedha ujao 2026/2027 Serikali imetenga zaidi ya bilioni 200 ili kununua vitendea kazi hivyo lengo likiwa ni kumaliza kabisa upungufu wa vitendea kazi vya usafiri kwa TANESCO katika maeneo yote nchini.

“Serikali iliwezesha TANESCO kuweza kunua Magari 556 kwa mwaka huu wa fedha 2025/2026 ili kurahisisha utoaji wa huduma ya umeme kwa wananchi, na kwa mwaka ujao wa fedha 2026/ 2027 Serikali imetenga zaidi ya bilioni 200 ili kununua vitendea kazi hivyo lengo likiwa ni kumaliza kabisa upungufu wa vitendea kazi vya usafiri kwa TANESCO”

Meneja wa TANESCO Mkoa wa Arusha Mhandisi Kisika Kisika amesema TANESCO katika Mkoa huo wamepokea vitendea kazi mbalimbali ikiwemo Magari makubwa 2, Gari aina ya Landcruser (4), Bajaji moja (1) vitakavyokwenda kuboresha zaidi huduma kwa wateja katika Mkoa huo.

“Tunaishukuru Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutupatia vitendea kazi hivi ambavyo kwa sasa tunakwenda kuvitumia kufikisha huduma kwa wananchi kwa haraka zaidi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.