DAR ES SALAAM.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb.) amewataka wajumbe wa Jukwaa la Ushindani la Afrika kuibua masuluhisho ya kivitendo, ambapo lengo kuu la ushirikiano huo liwe ni kutoa faida zinazoonekana kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kupata bidhaa na huduma bora kwa bei nafuu kupitia ushindani wa haki.
Amebainisha hayo wakati akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Ushindani la Afrika (ACF) jijini Dar es Salaam Aprili 13, 2026 ambapo amesema kuwa sera madhubuti za ushindani ndizo kiungo muhimu katika mabadiliko ya kiuchumi na kuongeza kuwa kuna ulazima wa nchi za Afrika kuoanisha sera zao za ushindani ili kuweka mazingira wezeshi ya biashara na kuchochea mapinduzi ya viwanda barani Afrika.
Mhe. Londo amesisitiza kuwa kadiri Afrika inavyozidi kuunganishwa kupitia Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), kuna haja ya haraka ya kuwa na sera za ushindani zenye mshikamano ili kudhibiti vitendo vinavyovuka mipaka vinavyoweza kukandamiza biashara.
Aidha amepongeza jukwaa hilo kwa kuimarisha uwezo wa mamlaka za ushindani na kuzuia ukiritimba ambapo juhudi hizo zinasaidia biashara ndogo na za kati (SMEs) kuingia sokoni na kushindana kwa usawa, jambo ambalo linaongeza uvumbuzi na tija.
Vilevile Mhe.Londo amesema Tanzania imejidhabiti kukuza utamaduni wa ushindani ili kufikia Dira ya Taifa ya mwaka 2050 na kuongeza kuwa serikali inaendelea kuimarisha taasisi za udhibiti ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Bi .Hadija Ngasongwa amesema Jukwaa hilo la ACF lenye nchi wanachama 37 ni madhubuti kwa ajili ya kusomana na kushirikiana na kujengeana uwezo hasa kwenye masuala yanayovuka mipaka baina ya nchi moja na nyingine ili kurahisisha utatuzi wa pamoja hata nje ya mipaka

Hakuna maoni: