TUZO YA TAIFA YA MWALIMU NYERERE YA UANDISHI BUNIFU YAFANA DAR, ABDILATIF ABDALLA AFUNGUKA

 


DAR ES SALAAM 

Mshairi maarufu duniani, Abdilatif Abdalla, amewataka waandishi bunifu kujitahidi kuinua viwango vyao kwa kujifunza mbinu mbalimbali za uandishi kupitia kazi za waandishi waliobobea.

Akizungumza katika hafla ya nne ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Julius Kambarage Nyerere ya Uandishi Bunifu, Abdalla alisema kuwa kusoma maandiko ya wengine humsaidia mwandishi kukuza uwezo wake na kumwezesha kujisimamia vyema katika taaluma hiyo.

Hafla hiyo ilifanyika usiku wa Aprili 13, 2026 katika ukumbi wa The Super Dome, jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa fasihi, sanaa na elimu kutoka ndani na nje ya nchi.

Aidha, Abdalla aligusia historia ya Julius Kambarage Nyerere akisema kuwa kama angekuwa hai, mwaka huu angeadhimisha miaka 104 tangu kuzaliwa kwake. Aliongeza kuwa siku yake ya kuzaliwa inafuatana kwa karibu na ya kiongozi huyo mashuhuri.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, alisoma shairi lililoandikwa na Julius Kambarage Nyerere, hatua iliyoongeza uzito wa kumbukumbu na heshima kwa mchango wake katika fasihi na taifa kwa ujumla.

Hafla hiyo ililenga kuenzi na kuhamasisha ubunifu katika uandishi wa Kiswahili na fasihi kwa ujumla. Kwa mujibu wa waandaaji, tangu kuanzishwa kwa tuzo hizo, jumla ya washindi 27 tayari wamewahi kutunukiwa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.