MRADI WA BILIONI 195.66 WA UJENZI MTO MSIMBAZI KUKUZA UCHUMI NA KUPUNGUZA ATHARI ZA MAFURIKO JIJINI DAR ES SALAAM
DAR ES SALAAM.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili 20, 2026, imesaini mkataba wa utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi wenye thamani ya shilingi bilioni 195.66, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti mafuriko na kuboresha mazingira ya makazi na shughuli za kiuchumi katika Jiji la Dar es Salaam.
Utekelezaji wa mradi huo utawezesha upatikanaji wa takribani hekta 57 za ardhi salama kwa ajili ya makazi na biashara, pamoja na ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo daraja jipya la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na karakana ya kisasa ya mabasi ya mwendokasi katika eneo la Ubungo Maziwa.
Aidha, ameiagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha maandalizi ya maeneo mbadala kwa ajili ya uhamishaji wa wafanyabiashara wanaoathirika na mradi huo yanafanyika kwa ufanisi, ili kulinda ustawi wao wa kiuchumi na kijamii.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ameeleza utayari wa serikali ya mkoa kuratibu kikamilifu utekelezaji wa mradi huo, akibainisha kuwa kipaumbele kitawekwa katika kuhakikisha wananchi wanaoathirika wanapatiwa maeneo mbadala yenye huduma muhimu ili kuepusha usumbufu katika maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Dar es Salaam Ilala Nurudin amesisitiza umuhimu wa mradi huo kwa maendeleo ya jiji, akieleza kuwa pamoja na kudhibiti mafuriko, pia utaongeza thamani ya ardhi, kuvutia uwekezaji na kuboresha taswira ya Dar es Salaam kama kitovu cha biashara na utalii.










Hakuna maoni: