Na Mwandishi Wetu,
Dodoma.
Waziri wa Nishati, Deogratus Ndejembi, amewahamasisha wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea maonesho ya Wiki ya Nishati 2026 yanayoendelea katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, yaliyoanza rasmi leo Aprili 20, 2026.
Akizungumza wakati wa ziara yake kwenye mabanda ya maonesho hayo, Mhe. Ndejembi amesisitiza umuhimu wa wabunge kutumia fursa hiyo kukutana na wataalamu wa sekta ya nishati ili kupata uelewa mpana kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati inayoendelea nchini.
Ameeleza kuwa maonesho hayo yanalenga kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya nishati chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, amesema maonesho hayo yanabeba ubunifu na teknolojia mbalimbali za nishati safi ya kupikia, zikiwemo majiko ya umeme, majiko mbadala, majiko ya gesi ya kuchomea nyama, pamoja na jiko maalum la umeme lililobuniwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa macho.
Maonesho hayo yanashirikisha taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Nishati, zikiwemo Shirika la Umeme Tanzania, Wakala wa Nishati Vijijini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli.
Katika ziara hiyo, Waziri Ndejembi aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Mha. Felchesmi Mramba.
Maonesho ya Wiki ya Nishati 2026 yanatoa jukwaa muhimu kwa wabunge na wadau mbalimbali kujifunza, kuona ubunifu, na kubadilishana uzoefu kuhusu maendeleo ya sekta ya nishati nchini.







Hakuna maoni: