Na Mwandishi Wetu,
Arusha.
WANANCHI wa Kijiji cha Losimingor, wilayani Monduli mkoani Arusha, wanatarajiwa kunufaika kiuchumi na kijamii kupitia utekelezaji wa Mradi wa Kujenga Ustahimilivu wa Bioanuai za Misitu ya Mazingira Asilia dhidi ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi (BUREFOBI), unaolenga kuunganisha uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya wananchi.
Mradi huo unatekelezwa katika vijiji vinavyopakana na Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Essimingor, ukiwa na lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi huku ukiboresha maisha ya jamii kupitia miradi ya maendeleo endelevu.
Losimingor ni miongoni mwa vijiji sita vinavyonufaika na mradi huo, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuleta mageuzi ya kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali ikiwamo uimarishaji wa majosho ya mifugo, sekta inayobeba maisha ya wananchi wengi wa eneo hilo.
Mbali na ufugaji, mradi huo pia unafungua fursa mpya za kipato kupitia utalii shirikishi, ambapo jamii itanufaika moja kwa moja kwa kushiriki katika shughuli za utalii, ikiwemo kuanzishwa kwa kituo cha jamii cha kuuza bidhaa za utalii. Hatua hiyo inalenga kupanua wigo wa ajira na kupunguza utegemezi wa moja kwa moja wa rasilimali za misitu.
Akizungumza Aprili 16,2026 wakati wa ziara ya timu ya mradi wilayani Monduli, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mwalimu Happiness Laizer, alisema halmashauri imejipanga kikamilifu kuhakikisha utekelezaji wa mradi unakuwa na tija kwa wananchi.
“Halmashauri ya Monduli inajivunia kuwa miongoni mwa wanufaika wa mradi huu. Tunaahidi tutatimiza wajibu wetu kikamilifu kadri tutakavyoelekezwa na wasimamizi wa mradi,” alisema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Someni Mteleka, alisema ziara hiyo inalenga kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi na kuhakikisha manufaa yaliyokusudiwa yanawafikia wananchi.
Alisisitiza kuwa TFS itaendelea kushirikiana na halmashauri za wilaya ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta matokeo chanya kwa jamii, huku ikiimarisha uhifadhi endelevu wa misitu.
Naye mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Getrude Lyatuu, alisema ushirikiano kati ya taasisi hiyo na TFS utaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na ushirikishwaji mpana wa jamii.
Alibainisha kuwa lengo kuu ni kuhakikisha makundi yote ya wananchi, wakiwemo wanawake na vijana, yanapata fursa sawa za kunufaika na miradi hiyo.
Ziara ya timu ya mradi inaendelea katika Mkoa wa Manyara, ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na tathmini ya athari zake kwa wananchi na mazingira.






Hakuna maoni: