Na Mwandishi Wetu,
Iringa.
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeanza kuonyesha msimamo mkali katika vita dhidi ya rushwa na ukiukwaji wa maadili kwa kuwataka watumishi wake kuzingatia kikamilifu nidhamu ya kazi na matumizi sahihi ya mifumo ya kiutumishi, hatua inayolenga kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utendaji.
Msisitizo huo umetolewa leo Aprili 16, 2026, katika siku ya pili ya semina ya mapambano dhidi ya rushwa na maadili kwa maafisa na askari wa Shamba la Miti Sao Hill, mkoani Iringa, ambapo watumishi wamekumbushwa wajibu wao wa kulinda rasilimali za umma kwa uadilifu.
Semina hiyo imewakutanisha watumishi wa TFS kwa lengo la kuimarisha uelewa wao kuhusu wajibu wa utumishi wa umma, hasa katika kuzingatia misingi ya uwazi, uadilifu na uwajibikaji wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Katika mafunzo hayo, washiriki wameelekezwa kwa kina juu ya umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, sambamba na matumizi sahihi ya mifumo ya kiutumishi ikiwamo Mfumo wa Upimaji Utendaji Kazi (PEPMIS), unaolenga kuongeza uwazi, ufanisi na ufuatiliaji wa utendaji wa watumishi.
Akizungumza katika semina hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi TFS na Meneja wa Rasilimali Watu, SAC Bahati Mtomaye, alisema matumizi sahihi ya Mifugo pamoja na kuzingatia maadili ni nguzo muhimu katika kuboresha utendaji wa taasisi na kujenga imani kwa umma.
“Ni muhimu kwa kila mtumishi kuzingatia maadili ya kazi na kutumia mifumo ya kiutumishi kama inavyotakiwa, kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuongeza uwajibikaji,” alisema.
Hatua hiyo ya TFS inakuja wakati Serikali ikiendelea kusisitiza uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa katika taasisi za umma, huku ikitaka watumishi kuwa mstari wa mbele katika kulinda rasilimali na kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.
Semina hiyo inaendelea kuwa kichocheo cha mabadiliko chanya kwa watumishi wa TFS katika Shamba la Miti Sao Hill, ikilenga kujenga utamaduni wa uwajibikaji, uadilifu na utendaji unaozingatia matokeo.







Hakuna maoni: