NDC NA JIMBO LA SICHUAN ZAINGIA MAKUBALIANO YA KIMKAKATI KUCHOCHEA MAPINDUZI YA VIWANDA NA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA 2050

 


Dar es Salaam, Tanzania

Aprili 21, 2026

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limesaini hati ya makubaliano ya kihistoria na Jimbo la Sichuan kutoka Jamhuri ya Watu wa China, yakilenga kuimarisha ushirikiano katika sekta za utafiti, uwekezaji na uendelezaji wa viwanda nchini. 

Makubaliano hayo yalisainiwa rasmi katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya NDC jijini Dar es Salaam, yakifungua ukurasa mpya wa mahusiano ya kimkakati kati ya pande hizo mbili katika safari ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt Nicolaus Shombe, alisema hatua hiyo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Tanzania katika kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani, unaojitegemea na unaoendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. 

Alieleza kuwa makubaliano hayo yataimarisha nafasi ya NDC kama kiunganishi muhimu kati ya rasilimali za asili na maendeleo ya viwanda, kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa na utaalamu wa hali ya juu kwa manufaa ya Watanzania.

Aidha, alibainisha kuwa ushirikiano huo utaongeza uwezo wa taasisi, kuboresha usimamizi wa rasilimali madini na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayosimamiwa na NDC, ikiwemo miradi ya chuma ya Liganga, makaa ya mawe na umeme ya Mchuchuma, pamoja na uendelezaji wa maeneo ya viwanda kama TAMCO na Kange, ambayo ni nguzo muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda. Kwa upande wake, 

Mkurugenzi Mkuu wa Maliasili wa Jimbo la Sichuan, Xu Zhiwen, alisisitiza kuwa makubaliano hayo yanafungua fursa mpya ya ushirikiano wa kina kati ya China na Tanzania, hususan katika sekta ya madini yenye umuhimu mkubwa kimkakati duniani. 

Alieleza kuwa hatua hiyo inaashiria mwanzo wa ushirikiano wa muda mrefu wenye mwelekeo wa utekelezaji wa miradi, huku akibainisha utayari wa Sichuan kushirikiana na Tanzania katika utafiti wa madini, maendeleo ya migodi ya kijani na kubadilishana utaalamu ili kufikia maendeleo ya pamoja. Kupitia makubaliano hayo, 

Pande zote zimekubaliana kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo utafiti na tathmini ya rasilimali madini ili kuboresha utambuzi na uthibitishaji wa akiba zilizopo, kuendeleza dhana ya migodi ya kijani inayozingatia uhifadhi wa mazingira, kutumia teknolojia za kisasa kama satelaiti na mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa ardhi na rasilimali, pamoja na kuendeleza maeneo ya viwanda kwa kutumia sayansi ya kisasa ya mipango ya maeneo.

 Aidha, makubaliano hayo yanajumuisha programu za mafunzo na uhamishaji wa teknolojia ili kujenga wataalamu wa Kitanzania wenye uwezo wa kushindana kimataifa.

Ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza uwekezaji, kuimarisha uhamishaji wa maarifa na teknolojia, na kuchochea kwa kasi ukuaji wa sekta ya viwanda na madini nchini. Vilevile, unalenga kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na rasilimali zake kwa njia endelevu, yenye tija na inayoongeza thamani ndani ya nchi.

Makubaliano haya yanaendana moja kwa moja na nguzo za Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuimarisha uchumi wa viwanda, kukuza matumizi ya sayansi na teknolojia, na kujenga uchumi jumuishi unaozalisha ajira na kuinua ustawi wa wananchi.

Pande zote mbili zimeonesha dhamira ya kujenga ushirikiano wa muda mrefu unaozingatia manufaa ya pamoja, uwazi na matokeo chanya yatakayochangia maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania na China kwa ujumla.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.