Na Mwandishi Wetu.
KATIKA kuadhimisha Siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi Duniani, ambayo kitaifa itafanyika Njombe Aprili 28 mwaka huu, Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) unatarajia kuendesha kliniki maalumu ya uchunguzi wa afya.
Kliniki hiyo inayojulikana kama Imarisha Afya na Mama Samia itahusisha uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kwa wananchi ikiwemo saratani, shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya wanawake, macho, mifupa pamoja na tathmini ya hali ya lishe. Aidha, wananchi watakaopima watapatiwa dawa katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema, Njombe.
Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alisema kuwa wamejipanga kuboresha huduma mwaka huu kwa kushirikisha madaktari bingwa na kutoa dawa, tofauti na miaka iliyopita ambapo walikuwa wakitoa ushauri na vipimo pekee.
Mwenda pia alitoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia huduma hiyo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, akishukuru Kampuni ya Dawa ya Planet kwa msaada wa dawa walioutoa.
Alisema maonesho hayo yatakayoanza Aprili 24 hadi 29 yatashirikisha zaidi ya kampuni 100 pamoja na wajasiriamali, jambo linalotarajiwa kuvutia wananchi wengi kujitokeza kupima afya na kupata ushauri pamoja na tiba.
“Tumekuwa tukitumia maadhimisho haya kutoa mafunzo, kufanya maonesho, kugawa vifaa kinga na kuendesha kliniki maalumu. Hivyo tunaomba wananchi wa Njombe na mikoa jirani wajitokeze kwa wingi,” alisema Mwenda.
Aliongeza kuwa kupitia programu ya Imarisha Afya na Mama Samia, OSHA imekuwa ikihudumia zaidi ya wananchi 5,000 kila mwaka, huku lengo la mwaka huu likiwa kuwafikia zaidi ya wananchi 10,000.
Kwa upande wake, Meneja Rasilimali wa Kampuni ya Dawa ya Planet, Andrew Paul, alisema msaada huo ni sehemu ya kurejesha shukrani kwa jamii inayowaunga mkono, na kuahidi kuendelea kushirikiana na OSHA katika kuboresha huduma kwa wananchi.




Hakuna maoni: