Na Mwandishi Wetu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka huu, ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Njombe.
Hayo yamesemwa leo Aprili 29, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alieleza kuwa maandalizi ya maadhimisho hayo yamekamilika.
Mtaka amesema mkoa umejipanga kikamilifu kumpokea kiongozi huyo mkuu wa nchi, na amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kiwanja kilichopo ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe kushiriki maadhimisho hayo.
Ameongeza kuwa maeneo yote muhimu yameimarishwa, hususan upande wa ulinzi na usalama, hivyo hakuna sababu ya wananchi kuwa na wasiwasi.
“Mei Mosi mwaka huu inafanyika hapa kwetu Njombe, na mgeni rasmi ni Rais Samia. Nawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kusherehekea pamoja na kiongozi wetu na wafanyakazi,” amesema Mtaka.
Aidha, ameeleza kuwa kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050”, hivyo ni muhimu kwa wananchi kushiriki ili kupata ujumbe wa maadhimisho hayo.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amesema maandalizi yao yako tayari na wana matumaini makubwa ya kusikia hotuba ya Rais Samia kuhusu maslahi ya wafanyakazi.
Amesema TUCTA itaendelea kuhamasisha wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza uzalishaji, hatua itakayosaidia kukuza mapato na uchumi wa taifa kwa ujumla.
“Najua wafanyakazi wanatarajia kusikia kuhusu nyongeza ya mishahara, lakini nawaomba tumsubiri Rais siku ya Mei Mosi,” amesema Nyamhokya.

Hakuna maoni: