RAIS SAMIA MGENI RASMI MKUTANO WA MAMA LISHE

DAR ES SALAAM. 

RAIS Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano mkubwa wa Mamalishe na Babalishe kutoka kote nchini utakaofanyika Aprili 11, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Mamalishe, Avijawa Omari, amesema kuwa kupitia Umoja wa Mamalishe na Babalishe Tanzania (UMALITA), wanaiomba serikali kuwatambua rasmi ili waweze kupata mikopo na fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazo wawezesha kujiajiri zaidi na pia kuajiri wengine.

Amesema mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu kwa mamalishe na babalishe kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa viongozi wa serikali, huku lengo kuu likiwa ni kuongeza kipato, kukuza biashara zao na kuchangia katika utoaji wa ajira nchini.

“Tunawaalika mamalishe na babalishe wote kujitokeza kwa wingi Aprili 11 katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere ili tushirikiane kujenga mustakabali wa biashara zetu,” amesema.

Aidha, ameeleza kuwa kaulimbiu ya mkutano huo ni “Pika Kishua, Vaa Kishua”, ikiwa na dhamira ya kuhamasisha maboresho ya huduma na hadhi ya kazi ya mamalishe na babalishe nchini.

“Mamalishe tumejiajiri na tunalisha taifa asubuhi, mchana, jioni na usiku. Tunaiomba jamii itambue mchango wetu na kutuheshimu kwa hadhi yetu,” ameongeza.

Pia amebainisha kuwa kundi hilo limepitia changamoto mbalimbali ikiwemo maradhi na mazingira magumu ya kazi, lakini sasa linaelekea kutumia nishati safi na mbinu bora zaidi za upishi ili kulinda afya na kuboresha biashara zao.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Babalishe, Ngosha, amesisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano kati ya wanachama ili kufanikisha malengo yao ya kiuchumi na kijamii.

Mkutano huo unatarajiwa kuwa wa kihistoria, ukileta pamoja wadau muhimu wa sekta isiyo rasmi na viongozi wa juu wa serikali kujadili mustakabali wa ajira na ujasiriamali nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.