SERIKALI YAAHIDI KUIWEZESHA OSHA KWA VITENDEA KAZI KUONGEZA UFANISI



Na Mwandishi Wetu, 

Njombe.

Serikali imeahidi kuendelea kuiwezesha Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) vitendea kazi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Deus Sangu, wakati akifunga maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Mjimwema, mkoani Njombe.

Waziri Sangu amesema OSHA ni taasisi muhimu katika kuhakikisha ufanisi wa wafanyakazi na usalama wao mahali pa kazi, hivyo serikali ina wajibu wa kuiwezesha kwa rasilimali zote muhimu.

“Hivyo serikali ina wajibu kuiwezesha OSHA kwa vitendea kazi vyote muhimu ikiwemo magari na vifaa vya ukaguzi,” amesema Waziri Sangu.

Ameongeza kuwa hadi sasa serikali imeipatia OSHA magari 50 pamoja na vifaa vya ukaguzi vyenye thamani ya shilingi bilioni saba.

Katika hatua nyingine, Waziri Sangu ameziagiza OSHA, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuhakikisha wanawabana waajiri wote kujisajili na kulipa michango pamoja na madeni wanayodaiwa.

Amesema licha ya kuwepo kwa zaidi ya waajiri 200,000 nchini, wale waliofikiwa na OSHA hawazidi 100,000, akisisitiza kuwa usajili wa OSHA ni takwa la kisheria na si hiari.

Kwa upande wa WCF, amesema baadhi ya waajiri katika sekta binafsi bado hawajawasajili wafanyakazi wao katika mfuko huo, huku akitoa siku 90 kwa waajiri hao kukamilisha usajili kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amewataka wafanyakazi kutoa taarifa endapo hawataona alama au mabango ya OSHA katika maeneo yao ya kazi.

“Hawa OSHA katika maeneo ya kazi ambayo yameshasajiliwa huweka mabango yao, hivyo kama hulioni ofisini kwako, toa taarifa ili hatua zichukuliwe,” amesema Nyamhokya.

Awali, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema katika maadhimisho hayo wamefanikiwa kuwafikia wajasiriamali 6,101 pamoja na maofisa usafirishaji 300 na kuwapatia vifaa kinga, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha mazingira salama ya kazi.

Amesisitiza kuwa OSHA itaendelea kutoa elimu, ushauri na uhamasishaji kuhusu masuala ya afya na usalama mahali pa kazi, hatua itakayosaidia kupunguza gharama kwa serikali na kuongeza uhimilivu wa mifuko ya wafanyakazi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.