Mtumba, Dodoma
Taasisi ya Wataalamu wa Mazingira Tanzania (TEEA) imeomba kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Madini ili kuhakikisha shughuli zote za utafutaji, uchimbaji na uchakataji wa madini nchini zinafanyika kwa kuzingatia misingi ya utunzaji na uendelezaji wa mazingira.
Ombi hilo limetolewa leo Aprili 1, 2026, katika ofisi za Wizara ya Madini zilizopo Mtumba jijini Dodoma, ambapo uongozi wa taasisi hiyo umefanya kikao na baadhi ya maafisa wa wizara hiyo kujadili namna bora ya kushirikiana katika kukabiliana na changamoto za kimazingira.
Katika kikao hicho, viongozi wa TEEA walitaja maeneo yanayochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira kuwa ni pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya maji, uharibifu wa ardhi unaotokana na uchimbaji holela, ukataji wa miti bila udhibiti, pamoja na matumizi ya kemikali hatarishi kama zebaki katika shughuli za uchimbaji mdogo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Mhandisi. Emmanuel Hanai amesema ushirikiano kati ya TEEA na Wizara ya Madini utatoa fursa pana kwa watumishi wa wizara hiyo kuongeza uelewa, maarifa na ujuzi kuhusu mbinu bora za uhifadhi wa mazingira, sambamba na kuimarisha utekelezaji wa sera na miongozo ya kimazingira.
Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017, TEEA imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali katika kuhamasisha na kusimamia masuala ya uhifadhi wa mazingira nchini.
“Kwa kuzingatia viwango bora vya kimazingira, tunaweza kuongeza thamani ya madini yetu na kuvutia uwekezaji zaidi, hali itakayowezesha sekta hii kuchangia mapato ya dola za Marekani kati ya milioni 50 hadi 100 kwa mwaka,” amesema Hanai.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi. Elias Kayandabila ameipongeza TEEA kwa wazo hilo, na amesema ni hatua muhimu itakayosaidia kuongeza ufanisi wa watumishi wa wizara hiyo, hususan wale wanaoshughulikia masuala ya mazingira moja kwa moja.
Ushirikiano huu unatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi katika usimamizi wa mazingira, huku ukilenga kuleta uwiano kati ya uchumi wa madini na uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.






Hakuna maoni: