Na Mwandishi Wetu,
Dodoma.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kati kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC), wameanza utekelezaji wa programu ya “Greening Railway Corridor” kwa kupanda miti 1,000 katika awamu ya kwanza ya miti 10,000 iliyopangwa kupandwa kando ya reli ya kati (MGR) na reli ya kisasa (SGR).
Mpango huo unalenga kurejesha uoto wa asili uliopotea wakati wa ujenzi wa miundombinu ya reli, sambamba na kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yanayozunguka reli.
Zoezi hilo la upandaji miti limefanyika kuanzia Aprili 9 hadi 16, 2026, likihusisha maeneo mbalimbali ya mwambao wa reli ya SGR katika stesheni za Samia Suluhu Hassan Dodoma, Igandu, Gulwe, Kidete, Kilosa na Mkata.
Aidha, katika reli ya kati (MGR), upandaji miti umefanyika katika stesheni za Dodoma na Kilosa, ambapo wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa taasisi hizo na wananchi wa maeneo husika walishiriki kikamilifu.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Mazingira wa TRC Makao Makuu, Mohamed Yusuph Mdeme, aliwataka wasimamizi wa stesheni (Station Masters) kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa ipasavyo kwa kuimwagilia, kuipalilia na kutoa huduma zote muhimu ili iweze kukua na kustawi kama ilivyokusudiwa.
Alieleza kuwa mafanikio ya programu hiyo hayatategemea tu upandaji miti, bali zaidi kwenye uendelevu wa utunzaji wake.
Kwa upande wa TFS, Mhifadhi wa TFS, Enos Samamba Enos, aliyeongoza zoezi hilo kwa niaba ya Kamanda wa Kanda ya Kati, alisema ushirikiano huo kati ya taasisi hizo ni hatua muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendana na uhifadhi wa mazingira.
Alibainisha kuwa TFS itaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuhakikisha miti inayopandwa inalindwa na kukua vizuri.
Katika zoezi hilo, miti ya aina ya Trichilia emetica (Mti maji) na Cordia sinensis (Mdawi) ilipandwa, ikiwa ni sehemu ya aina za miti inayostahimili mazingira ya ukanda husika.
Wananchi walioshiriki wamepongeza juhudi hizo wakisema zitachangia kuboresha mazingira, kuongeza kivuli na kuleta manufaa ya kiuchumi kwa jamii zinazozunguka maeneo ya reli.
Programu ya “Greening Railway Corridor” inatarajiwa kuendelea katika maeneo mengine ili kuhakikisha idadi iliyopangwa ya miti 10,000 inafikiwa na kuleta matokeo chanya kwa mazingira na jamii.





Hakuna maoni: