MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), unatarajia kuzindua lango la huduma binafsi kwa mfanyakazi na maombi maalumu ya simu yatakayojulikana kama WCF Mkononi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk. John Mduma, wakati akizungumza katika Mkutano Maalumu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulioitishwa kwa lengo la kujadili mapendekezo ya marekebisho ya Katiba ya jukwaa hilo.
Mkurugenzi huyo amesema WCF imewekeza kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kuhakikisha utekelezaji thabiti wa majukumu na utoaji wa huduma, unakuwa na ufanisi.
Amesema hadi sasa zaidi ya asilimia 95 ya huduma wanazozitoa zinapatikana kwa mtandao, ikiwa ni pamoja na kusajili wanachama, ukusanyaji wa michango, uwasilishaji na uchakataji wa madai hadi malipo ya fidia.
Dk. Mduma amesisitiza katika kutatua changamoto hiyo wameamua kuja na lango la huduma binafsi kwa mfanyakazi na maombi maalum ya simu inayojulikana kama WCF Mkononi ambayo wataizindua hivi karibuni.
Amesema kupitia mfuko huo mfanyakazi utaweza kupata huduma za kuboresha taarifa zake binafsi, kuangalia l taarifa ya michango yake inavyowasilishwa na mwajiri wake WCF, kufuatilia madai yake ya fidia, kuona na kupakua barua na kutoa maoni.
Dk. Mduma amesema wanaamini matumizi ya mifumo hiyo yatakapoanza hivi karibuni, wafanyakazi wataweza kufahamu michango yao ya kila mwezi na kusaidia kufuatilia kwa waajiri wao kuhusu utekelezaji wa takwa hilo la kisheria.
"Kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi anayepaswa kuchangia ni mwajiri ambaye anatakiwa kuwasilisha WCF asilimia 0.5 ya mshahara wa kila mfanyakazi wake; na ndio maana hata mkiangalia katika zile ‘salary slips’ zenu hamuoni michango iliyopelekwa WCF.” amesema.


Hakuna maoni: