DAR ES SALAAM
Wamiliki wa ardhi nchini wametakiwa kulipa pango la ardhi ndani ya siku 14 kuanzia Aprili 24, 2026, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukrani Kyando, amesema ulipaji wa kodi ya ardhi ni wajibu wa msingi kwa kila mmiliki wa ardhi kwa mujibu wa sheria za nchi, na haupaswi kupuuzwa.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 24(1), haki ya kumiliki ardhi inaambatana moja kwa moja na wajibu wa kulipia pango la ardhi kama inavyoelekezwa na sheria husika.
Kyando amebainisha kuwa ukaguzi uliofanyika kwa zaidi ya wananchi 600 umeonyesha kuwa idadi kubwa bado haijalipa kodi hiyo kwa zaidi ya miezi mitatu, licha ya kupewa elimu na kukumbushwa mara kwa mara juu ya umuhimu wa kutekeleza wajibu huo.
Amesisitiza kuwa baada ya kipindi cha wiki mbili kumalizika, serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria, ikiwemo kuwachukulia hatua mahakamani wale wote watakaokiuka agizo hilo.
“Kila mmiliki wa ardhi anatakiwa kulipa pango la ardhi kwa mujibu wa sheria, hivyo ni vyema wananchi wakazingatia wajibu huu ili kuepuka usumbufu wa kisheria,” ameeleza.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kodi Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Lihapa, amewahimiza wamiliki wa viwanja kulipa kodi hiyo kwa wakati, akieleza kuwa kufanya hivyo kutasaidia kuepusha adha zisizo za lazima.
Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, Sura ya 113 kifungu cha 35(a), ulipaji wa kodi ya ardhi ni takwa la kisheria ambalo kila mmiliki anatakiwa kulitekeleza.
Aidha, ameonya kuwa serikali itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria hiyo na haitasita kuchukua hatua kwa wale watakaoshindwa kulipa kwa hiari.
Amesisitiza kuwa ulipaji wa kodi ya ardhi si hiari bali ni wajibu unaotakiwa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria, na kwamba kufanya hivyo kwa wakati husaidia serikali kuboresha huduma za kijamii pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ardhi nchini.


Hakuna maoni: