Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Chama cha ACT Wazalendo kimeitangazia umma maazimio ya kikao cha dharura cha Kamati Kuu kilichofanyika Mei 3, 2026, ambapo kimeendelea kusisitiza msimamo wake wa kuikataa Ripoti ya Tume ya Jaji Chande iliyochunguza matukio ya mauaji ya Oktoba 2025.
Maazimio hayo yameelezwa a na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Isihaka Mchinjita, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo amesema ripoti hiyo imeshindwa kuwawajibisha wahusika wa mauaji na badala yake imeelekea kuwasafisha.
Ameongeza kuwa hata takwimu zilizotolewa na tume zinaonesha zaidi ya watu 518 waliuawa, lakini hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa dhidi ya waliohusika, jambo alilodai linaibua maswali juu ya dhamira ya tume hiyo.
Mchinjita aliongeza kuwa tume hiyo imewatia hatiani wananchi kwa madai ya kupanga vurugu badala ya kushughulikia chanzo halisi cha mgogoro, ikiwemo kile alichokiita dhulma ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akieleza kuwa tume pia imeshindwa kubainisha wazi waliohusika na mauaji hayo.
Kutokana na hali hiyo, alieleza kuwa ACT Wazalendo inapendekeza kuanzishwa kwa uchunguzi huru wa kimataifa chini ya taasisi kama Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika au SADC, pamoja na kuachiwa huru kwa watu wote wanaoshikiliwa kwa sababu za kisiasa.
Aidha, alitoa wito wa kuwajibishwa kwa viongozi mbalimbali wa vyombo vya dola na serikali wanaodaiwa kuhusika na matukio hayo, sambamba na kusisitiza umuhimu wa kuanza mchakato wa Katiba Mpya na kufanya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi ili kuhakikisha haki na uwazi nchini.
Katika hitimisho lake, Mchinjita alionya kuwa taifa linakabiliwa na uchaguzi kati ya njia ya haki na uwajibikaji au kuendelea na ukandamizaji, akisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kusimama upande wa ukweli, haki na utawala wa sheria kwa mustakabali wa nchi.

Hakuna maoni: