BALOZI WA TANZANIA NCHINI UFARANSA AHIMIZA USAWA WA KIJINSIA KATIKA ELIMU YA JUU

Paris, Ufaransa.

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, amekutana na ujumbe wa viongozi wanawake 18 kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) waliopo nchini Ufaransa kwa ziara ya kitaaluma ya kujenga uwezo na kubadilishana uzoefu kuhusu uongozi, usimamizi wa taasisi za elimu ya juu na maendeleo ya wanawake katika nafasi za maamuzi.

Ujumbe huo unaongozwa na Dkt. Janeth Emanuel Kigoba, Mkuu wa Kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, ambaye pamoja na viongozi wengine wanashiriki programu mbalimbali za kujifunza na kutathmini mifumo bora ya uongozi na utawala katika taasisi za elimu ya juu.

Akizungumza na ujumbe huo katika Ubalozi wa Tanzania mjini Paris, Balozi Yakubu alisema imekuwa jambo la kutia moyo kuona kuwa sekta ya elimu ya juu, ambayo kwa miaka mingi imekuwa nyuma katika kufikia usawa wa kijinsia ikilinganishwa na baadhi ya sekta nyingine, sasa inaendelea kupiga hatua na kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

“Nimefarijika kuona idadi kubwa ya wanawake viongozi kutoka taasisi ya elimu ya juu wakishiriki katika programu za kujijengea uwezo. Elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii, hivyo ni muhimu kuona wanawake wakichukua nafasi zao stahiki katika kuongoza taasisi hizi muhimu,” alisema Balozi Yakubu.

Aliongeza kuwa vyuo vikuu vina nafasi ya kipekee katika kuandaa viongozi, wataalamu na watunga sera wa kesho, hivyo kuwepo kwa usawa wa kijinsia katika sekta hiyo kuna mchango mkubwa katika kuharakisha maendeleo ya taifa na jamii kwa ujumla.

Balozi Yakubu aliwahimiza washiriki hao kuendelea kuwa vinara wa mabadiliko katika taasisi zao kwa kuhakikisha kuwa wanawake wengi zaidi wanapata fursa za kushiriki katika uongozi, utafiti na ufundishaji.

Kwa upande wake, Dkt. Janeth Emanuel Kigoba alimshukuru Balozi Yakubu na Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa kwa mapokezi na ushauri walioutoa kwa ujumbe huo, akisisitiza kuwa ziara hiyo imewapa washiriki fursa muhimu ya kujifunza uzoefu wa kimataifa unaoweza kusaidia kuimarisha utendaji na uongozi wa taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Chuo Kikuu Huria cha Tanzania za kuimarisha uwezo wa viongozi wanawake na kukuza ushiriki wao katika nafasi za juu za uongozi, sambamba na kuchochea maendeleo ya elimu ya juu na usawa wa kijinsia nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.