KAGERA.
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania (EWURA) imesema imeridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ikieleza kuwa kasi ya ujenzi inaashiria uwezekano wa kuanza kwa usafirishaji wa mafuta ndani ya muda uliopangwa.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Ngosi Mwihava, amesema hayo kwa niaba ya wajumbe wa bodi hiyo walipotembelea sehemu ya mradi katika Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera kwa lengo la kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati unaounganisha Uganda na Tanzania.
Amesema bodi hiyo imevutiwa na namna mkandarasi anavyotekeleza mradi kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu, ratiba ya utekelezaji pamoja na masharti ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii zinazozunguka mradi.
“EWURA ndiyo iliyotoa kibali cha ujenzi wa bomba hili kwa upande wa Tanzania, na ziara hii ambayo ilianzia Dodoma imelenga kuhakikisha yale yote tuliyokubaliana, ikiwemo utunzaji wa mazingira, utoaji wa kipaumbele cha ajira kwa Watanzania na maeneo mengine, yanatekelezwa,” amesema Mwihava.
Ameongeza kuwa EWURA pia itahusika kutoa vibali vya kuanza kazi ya usafirishaji wa mafuta ghafi kupitia Tanzania mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya mradi huo.
“Tumeshuhudia kazi kubwa ikiendelea kwa kasi ya kuridhisha. Maendeleo haya yanaonyesha kuwa matarajio ya kuona mafuta yakianza kusafirishwa kupitia bomba hili yanaweza kufikiwa ndani ya muda uliopangwa,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mradi wa EACOP umefikia zaidi ya asilimia 70 ya utekelezaji, huku shughuli mbalimbali zikiendelea kwa kasi katika maeneo tofauti, ikiwemo Chongoleani mkoani Tanga ambako ujenzi wa matenki ya kuhifadhia mafuta umekamilika na majaribio yanaendelea.
Katika eneo la Chongoleani pia kuna ujenzi wa gati la kusafirisha mafuta kwenda nje ya nchi mara baada ya mradi huo kuanza rasmi kazi.
Mwihava amesema pamoja na umuhimu wa mradi huo katika sekta ya nishati, utekelezaji wake umeendelea kuleta manufaa kwa wananchi kupitia ajira, huduma za kijamii na fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wazawa wanaoishi katika maeneo yanayopitiwa na bomba hilo.
“Tumefurahishwa kuona kuwa masuala ya mazingira yanazingatiwa kwa umakini mkubwa. Aidha, jamii zinazozunguka mradi zimeendelea kushirikishwa na kunufaika kupitia miradi ya kijamii pamoja na ajira zinazotokana na utekelezaji wa mradi,” ameongeza.
Hata hivyo, amewataka wakandarasi na kampuni zinazoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo kuendelea kuzingatia masharti yaliyowekwa na mamlaka za usimamizi, hususan kuongeza ushiriki wa wazawa katika shughuli mbalimbali za mradi.
Amesisitiza kuwa Serikali ina matarajio makubwa kuona Watanzania wengi zaidi wakipata ajira, mafunzo ya ujuzi na fursa za biashara kupitia mradi huo unaotajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mradi wa EACOP unahusisha ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, ambapo sehemu kubwa ya bomba hilo inapita nchini Tanzania.
Mradi huo unamilikiwa na TotalEnergies kwa asilimia 62, huku Tanzania Petroleum Development Corporation na Uganda National Oil Company kila moja likimiliki asilimia 15, na CNOOC ikimiliki asilimia 8.

Hakuna maoni: