BONDIA MASHUHURI CRAWFORD ATEULIWA KUWA BALOZI WA UTALII TANZANIA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.), Leo Mei 28, 2026 amemteua Bondia mashuhuri kutoka Marekani, Terence “Bud” Crawford kuwa Balozi wa Utalii wa Tanzania

Akiwa katika ziara yake Hifadhi ya Taifa Serengeti, alikutana na Bondia huyo aliyekuwa akifanya Royal Tour katika Hifadhi hiyo, Dkt. Kijaji amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuendelea kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kimataifa kupitia watu mashuhuri.

Amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana kutokana na filamu za Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania zilizoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yameendelea kuvutia wageni mbalimbali duniani, wakiwemo wanamichezo maarufu.

“Moja ya mbinu tunazotumia ni kushirikiana na watu mashuhuri ili kuendeleza kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Rais Samia katika kutangaza utalii wetu. Tumemteua Terence Crawford kuwa balozi wa hiyari wa utalii ili akatangaze vivutio alivyojionea hapa nchini,” alisema Dkt. Kijaji.

Ameongeza kuwa michezo ni sekta muhimu inayochangia ajira na kuunganisha watu kutoka mataifa mbalimbali, hivyo Watanzania wanapaswa kuwahamasisha watoto kushiriki michezo kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

“Kama taifa, Rais Samia amewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya michezo. Ni muhimu wazazi na jamii kuwapeleka watoto katika shule za michezo ili kuzalisha wanamichezo watakaoweza kutumia fursa zinazojitokeza kupitia sekta hii.” Alisema Dkt. Kijaji

Aidha, Dkt. Kijaji aliongeza “tunawaona akina Terence wakija Tanzania, akina Rio Ferdinand (mwanasoka wa zamani wa England ) wakija, hivyo Watanzania tuipe nafasi kubwa sekta hii ya michezo kwa kuwa inatuunganisha na mengi ndani ya taifa letu na nje ya taifa letu.”

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.