DODOMA.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amewasilisha makadirio ya Bajeti ya wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Katika hotuba yake leo Mei 22, 2026, Mhe. Kapinga ameanika mafanikio na maendeleo ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) katika kurahisisha mazingira ya biashara nchini.
Waziri Kapinga amesema kuwa kufikia Aprili 2026, BRELA imefanikiwa kusajili kampuni 16,864, sawa na asilimia 86 ya lengo la kusajili Kampuni 19,640, pamoja na Majina ya Biashara 30,631, ikiwa ni asilimia 91 ya lengo. Kasi hiyo inaonyesha kuwa ari ya Watanzania kurasimisha biashara zao imeongezeka kwa kiwango kikubwa.
Aidha, BRELA ilisajili Alama za Biashara na huduma 2,804, sawa na asilimia 78 ya lengo, pamoja na kutoa Vyeti vya Usajili wa Viwanda 42. Kwa upande wa Hataza (Patent), Wakala umevuka lengo kwa kufikia asilimia 110 baada ya kutoa Hataza 44 kati ya 40 zilizopangwa.
Sambamba na hilo, BRELA imetoa Leseni za Viwanda 512, ikivuka lengo la leseni 437 kwa asilimia 117 ya utekelezaji. Pia, jumla ya Leseni za Biashara kundi “A” 19,110 zilitolewa, sawa na asilimia 89 ya lengo.
“Kufikia Aprili 2026, Wakala imezuia Uhuishaji wa Leseni za Biashara 901. Kati ya hizo, Leseni 737 ni za Biashara za uingizaji wa Bidhaa, Leseni tano ni za huduma za Posta na utoaji wa vifurushi ndani ya Mipaka ya Taifa, Leseni 119 ni za uwakala au udalali katika Sekta ya mali isiyohamishika, na Leseni 86 ni za huduma za usafirishaji wa Shehena. Hatua hii imerejesha Imani ya wazawa kwa Serikali kwa namna inavyosaidia kutatua changamoto za Biashara, imeboresha mazingira ya Biashara kwa Wazawa na hivyo kuongeza uwekezaji na uwezo kwa ushindaji wa wazawa kwenye Biashara” Alisema Waziri Kapinga
Waziri Kapinga alisisitiza kuwa mageuzi ya BRELA yamefikia pia ukaguzi wa Wamiliki Manufaa (Beneficial Ownership), ambapo kampuni 632 zilitembelewa katika Mikoa ya Dar es Salaam na Arusha. Kati ya hizo, Kampuni 398 sawa na asilimia 63 ziliwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa, huku Kampuni 562 sawa na asilimia 89 zikiwa zimelipa ada za mwaka (Annual Returns). Hatua hiyo inaonyesha kuongezeka kwa uwazi na uaminifu katika Sekta ya Biashara Nchini.
Katika kurahisisha mazingira ya kufanya Biashara Nchini, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wadau wengine imeendelea kufanya mapitio ya Sheria mbalimbali. Sheria zilizofanyiwa mapitio ni pamoja na Sheria ya Kampuni Sura ya 212, Sheria ya Majina ya Biashara Sura ya 213, Sheria ya Alama za Biashara na Huduma Sura ya 326, Sheria ya Usajili wa Hataza Sura ya 217, na Sheria ya Alama za Bidhaa Sura ya 85. Mapitio ya Sheria hizi zote yamekamilika na zipo katika hatua za uidhinishwaji.
Katika mwaka wa Fedha 2026/2027, Wizara ya Viwanda na Biashara imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 137,812,633,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 104,122,530,000 ni kwa matumizi ya kawaida, ambapo Shilingi 78,049,345,000 ni mishahara na Shilingi 26,073,185,000 ni matumizi mengineyo. Aidha, Shilingi 33,690,103,000 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, huku fedha zote za maendeleo zikiwa ni za ndani.

Hakuna maoni: