DAS KIGAMBONI AZINDUA OFISI YA WILAYA YA KITANESCO YA KIMBIJI



DAR ES SALAAM. 

Katibu Tawala Wilaya ya Kigamboni Bi. Upendo Mahalu amezindua Ofisi mpya ya Wilaya ya KiTANESCO Kimbiji ikiwa ni mkakati wa Shirika wa kuendelea kuwahudumia na kusogeza huduma zake karibu na wananchi.

Akizungumza Mei 04, 2026 kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bi. Upendo Mahalu, amesema uzinduzi wa Ofisi hiyo umelenga kuboresha utoaji huduma kwa wananchi kadri mahitaji ya nishati ya umeme yanavyozidi kuongezeka.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inaakisi maboresho ya kiutendaji yanayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto ya umbali kwa wananchi ambao hapo awali walilazimika kufuata huduma katika ofisi za mkoa zilizopo Tungi Mnadani.

“Lengo la uzinduzi huu ni kuboresha huduma kwa wananchi na kuendana na kasi ya ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme kwa maendeleo ya nchi. Naipongeza Menejimenti ya TANESCO kwa maono ya kusogeza huduma karibu na wananchi,” alisisitiza Bi. Mahalu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Mhe. Haran Sanga, ameipongeza TANESCO kwa maboresho makubwa ya kiutendaji na kimtazamo, huku akiwataka wananchi kuwa mstari wa mbele kulinda miundombinu ya umeme, akisisitiza kuwa serikali inawekeza fedha nyingi katika sekta hiyo.

Akizungumza Kaimu Meneja Huduma kwa Wateja, Bw. Shamu Lameck, amesema TANESCO inaendelea kuimarisha huduma zake kwa wateja kwa kutoa elimu na taarifa sahihi kuhusu matumizi ya umeme na miundombinu yake.

“Dhamira yetu ni mteja kwanza. Tunaendelea kuongeza juhudi kuhakikisha kila mteja anafikiwa na huduma bora ya umeme, tunaishukuru sana Serikali kwa kutaoa ushirikiano katika kufikia malengo yetu ya kumuhudumia mteja kwa ufanisi,” alieleza.

Ofisi ya TANESCO Kimbiji itahudumia kata za Kimbiji, Somangila, Pembamnazi na Kisarawe II. Uzinduzi huo pia uliambatana na kukabidhiwa kwa vitendea kazi, yakiwemo magari na bajaji yatakayosaidia kuwafikia wateja kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.