Na Mwandishi Wetu, Mikumi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, leo Mei 2, 2026, ametembelea Hifadhi ya Taifa Mikumi kukagua uwekezaji wa miundombinu ya kuendeleza utalii Hifadhi ya Taifa Mikumi ikiwemo pia kujionea kukamilika kwa hoteli ya kisasa iitwayo Mikumi Wildlife Lodge.
Amesema uwekezaji wa uwanja wa ndege wa kisasa sasa utakamilika ndani ya mwaka huu baada ya kupatikana mkandarasi mpya ambapo utawekewa lami maalum (polymer) na utakuwa na majengo ya kisasa ya kuwasili na kuondokea watalii.
“Ukamilishaji wa uwanja huu wa kisasa ulipata changamoto kidogo lakini sasa tumezitatua na azma ya nchi kuona watalii wanatua kwenye uwanja mpya inakwenda kutimia ndani ya miezi sita ijayo kwani mkandarasi mpya ameanza kazi na leo nimejionea yuko kazini na vifaa vyote,” alisema Dkt. Abbasi.
Kwa upande mwingine Dkt. Abbasi ametembea na kujionea kuendelea kukamilika kwa Hoteli ya Wellworth Mikumi Wildlife Lodge ambayo imeboreshwa chini ya uwekezaji binafsi na sasa imeanza kupokea wageni ikiwa na vyumba 48 vya kisasa, chumba cha mazoezi cha kisasa (gym), sehemu za michezo, ukumbi wa kisasa wa mikutano, bwawa la kuogelea na mandhari ya kuvutia.
“Uwekezaji huu nao ni mfano hai namna sekta binafsi yenye tija inavyoweza kushirikiana na Serikali kuendeleza sekta ya utalii. Nawapongeza kampuni ya Wellworth kwa uwekezaji huu wa kihistoria,” alisema.









Hakuna maoni: