EFTA YATOA TUMAINI LA UKOMBOZI WA KIUCHUMI KWA WANANCHI



DAR ES SALAAM.

Mafanikio ya hatifungani ya kampuni ya Equity for Tanzania (EFTA) kuvuka zaidi ya mara mbili ya lengo lake la ukusanyaji wa fedha yameelezwa kuwa ishara ya kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa ndani katika masoko ya mitaji nchini.

Hayo yamebainishwa wakati wa Hafla ya kuorodheshwa rasmi kwa hatifungani hiyo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ambapo Mkurugenzi wa EFTA, Nicomed Bohay, alisema hatua hiyo si tu imeongeza mtaji wa kampuni, bali pia imeongeza hadhi ya Tanzania katika sekta ya uwekezaji na masoko ya mitaji.

Alisema ushiriki mkubwa wa wawekezaji unaonesha namna wananchi wanavyoendelea kuamini mifumo rasmi ya uwekezaji, huku akisisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuendelea kubuni mbinu mbalimbali za kiuchumi zitakazosaidia kuikomboa jamii dhidi ya umasikini.

“Katika kujikwamua na kuikomboa jamii yetu kiuchumi ni lazima kuendelea kubuni njia mbalimbali za uwekezaji kama hizi ili wananchi waweze kushiriki moja kwa moja katika kukuza uchumi,” alisema Bohay.

Aliongeza kuwa bodi ya EFTA itaendelea kujidhatiti katika usimamizi wa vihatarishi (risk management) pamoja na kuhakikisha fedha zote zilizokusanywa zinatumika katika maeneo yenye tija na yaliyokusudiwa ili kuleta manufaa kwa wawekezaji na jamii kwa ujumla.

Bohay pia aliwashukuru washauri wakuu na wadhamini wa EFTA, akiwemo Benki ya CRDB, kwa mchango wao mkubwa uliofanikisha hatifungani hiyo kupata mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, aliipongeza EFTA kwa kufanikiwa kuvuka lengo lake la ukusanyaji wa fedha kutoka shilingi bilioni 15 hadi zaidi ya shilingi bilioni 33.

Alisema mafanikio hayo yanaonesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika masoko ya mitaji nchini pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyoendelea kuwekwa na serikali.

CPA Mkama alisema asilimia 95.4 ya walioshiriki katika uwekezaji huo ni wawekezaji binafsi huku asilimia 4.4 wakiwa taasisi mbalimbali.

Aidha, alisema asilimia 99 ya wawekezaji wote ni wa ndani, huku asilimia iliyobaki ikiwa ni wawekezaji wa kigeni, jambo alilosema linaashiria mwamko mkubwa wa Watanzania kushiriki katika uwekezaji kupitia masoko ya mitaji.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.