HUDUMA YA APITHERAPY YAVUTIA VIONGOZI MAONESHO YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII BUNGENI

Dodoma

Huduma ya tiba asilia ya udungwaji wa nyuki maarufu kama Apitherapy imeendelea kuwa kivutio kikubwa katika banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwenye maonesho ya Wizara ya Maliasili na Utalii yanayoendelea katika viunga vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma.

Idadi kubwa ya viongozi wanaotembelea banda hilo wameonesha kuvutiwa na huduma hiyo kwa kupata elimu na ufafanuzi kuhusu matumizi ya sumu ya nyuki katika tiba mbalimbali za asili, huku baadhi yao wakiamua kupata huduma hiyo mara moja baada ya maelezo.

Huduma hiyo ya tiba asilia hutumia sumu ya nyuki kwa lengo la kusaidia kuimarisha kinga ya mwili na kupunguza baadhi ya matatizo ya kiafya. Katika huduma hiyo, nyuki huwekwa kwenye maeneo maalum ya mwili ili kumdunga mhudumiwa, au hutumika bidhaa zilizochakatwa kitaalamu zenye sumu ya nyuki.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mhifadhi wa TFS na Afisa Nyuki kutoka Hifadhi ya Mazingira Asilia Vikindu, Brenda Mwakipesile, alisema huduma hiyo imekuwa ikisaidia watu wenye changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo arthritis, rheumatism pamoja na maumivu ya viungo na misuli.

Alisema pia sumu ya nyuki inaweza kusaidia kuchochea mzunguko mzuri wa damu mwilini pamoja na kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili.

“Baadhi ya watu waliopata tiba hii wameripoti kupata nafuu ya maumivu, utulivu wa mwili na akili pamoja na kupungua kwa msongo wa mawazo na uchovu,” alisema Brenda.

Aidha, alieleza kuwa bidhaa zitokanazo na nyuki hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali za ngozi zinazosaidia kuboresha afya ya ngozi, hususan kwa watu wenye matatizo sugu ya ngozi.

Maonesho ya Wizara ya Maliasili na Utalii yameendelea kutoa fursa kwa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuonesha huduma, bidhaa na ubunifu mbalimbali unaolenga kuhifadhi rasilimali za asili pamoja na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.