IZO MOTORS YAZINDUA BETRI ZENYE UBORA WA JUU TANZANIA


DAR ES SALAAM. 


Kampuni ya IZO Motors Company Limited imezindua rasmi biashara ya betri za magari zinazojulikana kwa jina la IZO Battery, huku ikiahidi kutoa bidhaa zenye ubora wa hali ya juu kwa watumiaji nchini Tanzania.

Akizungumza kuhusu uzinduzi huo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Izo Mahemge, amesema betri hizo zimeandaliwa kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyolenga kuhakikisha uimara, uwezo mkubwa wa kuhifadhi na kutoa nguvu pamoja na kudumu kwa muda mrefu katika mazingira mbalimbali ya matumizi.

Amesema kampuni hiyo yenye makao yake makuu Kariakoo jijini Dar es Salaam inalenga kuwafikishia Watanzania bidhaa bora kwa bei nafuu pamoja na huduma ya ushauri sahihi kuhusu matumizi ya betri na matairi ya magari.

Kwa mujibu wa Mahemge, kampuni hiyo tayari imeanza usambazaji wa bidhaa zake katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wateja wa mijini na vijijini wanapata huduma kwa haraka na uhakika zaidi.

Katika hatua nyingine, kampuni hiyo imemtangaza msanii na mshawishi wa masuala ya magari mitandaoni, Dotto Magari, kuwa balozi rasmi wa bidhaa za IZO Battery, hatua inayotajwa kuongeza nguvu katika kuitangaza bidhaa hiyo kwa wananchi.

Izo Mahemge amesema uteuzi wa Dotto Magari umetokana na ushawishi wake mkubwa kwa jamii hususan kwa vijana na wadau wa sekta ya magari, ambapo anaamini ushirikiano huo utaongeza uelewa wa watu kuhusu ubora na matumizi sahihi ya betri hizo.

Kwa upande wake, Dotto Magari amesema anafurahishwa na ushirikiano huo na kuahidi kuitangaza IZO Battery kwa nguvu zote kutokana na ubora wa bidhaa hiyo pamoja na dhamira ya kampuni ya kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Amesema kupitia jukwaa lake kubwa la mitandao ya kijamii ataendelea kuwahamasisha wananchi kutumia bidhaa zenye ubora na zinazodumu kwa muda mrefu, huku akiitaka jamii kuunga mkono bidhaa zinazolenga kutoa suluhisho sahihi kwenye sekta ya magari.

Aidha, kampuni hiyo imewaalika wadau mbalimbali, wafanyabiashara, madereva pamoja na wananchi kutembelea ofisi zao zilizopo Kariakoo, Narung’ombe na Lumumba jijini Dar es Salaam ili kujionea huduma na bidhaa zinazotolewa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.