JAB YAWEKA SHARTI LA ITHIBATI SAMIA KALAMU 2026

 

Na Mwandishi Wetu

Waandishi wa Habari watakaoshiriki Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za Maendeleo (Samia Kalamu Awards - SKA) 2026 wamelazimika kukidhi sharti la kuwa na ithibati kutoka Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), hatua inayolenga kuimarisha weledi, uwajibikaji na ushindani wa haki katika taaluma hiyo.

Akizindua rasmi mchakato wa kupokea kazi za kushindanishwa, Jumapili Tarehe 31 Mei, 2026, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa SKA, Mha. Peter Mwasalyanda, amesema maandalizi ya mwaka huu yanazingatia maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kutambua mchango wa Waandishi wa Habari za maendeleo nchini.
Mwasalyanda amesema ili kuhakikisha uadilifu, uwazi na ushindani wa haki, maandalizi ya tuzo hizo yanahusisha pia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kama mdau muhimu katika kusimamia weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

“Tuzo hizi zinalenga kutambua, kuthamini na kuhamasisha uzalishaji wa maudhui ya ndani yenye ubora, yanayochangia kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha, na kuimarisha taswira chanya ya Taifa kupitia habari za maendeleo,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesema tofauti na msimu wa kwanza wa tuzo hizo, mwaka huu washiriki wanapaswa kuhakikisha wamekidhi sharti la ithibati.

“Mtakumbuka Msimu wa kwanza wa Samia Kalamu mambo ya JAB hayakuwepo, kwa hiyo waandishi walishiriki wote bila kujali vigezo vya Ithibati lakini mwaka huu kuna hiki kigezo cha kuwa na ithibati kwa hiyo niwashauri basi wote wanaoshiriki kwenye hizi tuzo wahakikishe wanakuwa na ithibati, wamethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.” Amesema Wakili Kipangula na kuongeza;
“Ni muhimu sana kwa sababu ni takwa la kisheria na kitu ambacho hatuwezi kukikwepa. Nawahamasisha tushiriki wote kwa sababu isionekane ni tuzo za watu fulani tu, kila mmoja awasilishe kazi zake,” amesema Kipangula.

Kwa mujibu wa vigezo vya ushiriki vilivyotangazwa, Waandishi wa Habari wa Tanzania Bara wanatakiwa kuwa wamethibitishwa na JAB, huku kwa Zanzibar washiriki wakitakiwa kuwa na kitambulisho cha Mwandishi wa Habari (Press Card).

Tuzo hizo zimeanza kupokea kazi kuanzia Mei 31 hadi Juni 30, 2026 na zinatarajiwa kutolewa kati ya Oktoba na Desemba mwaka huu.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.