Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ufalme wa Ubelgiji zimefanya mazungumzo yaliyolenga kupitia maendeleo ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo pamoja na kujadili maeneo ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mazungumzo hayo yamefanyika Mei 22, 2026 katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, yakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bi. Ellen Maduhu pamoja na Balozi wa Ubelgiji nchini, Mhe. Peter Huyghebaert.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano hususan katika sekta za elimu, biashara, uwezeshaji wa vijana na wanawake, taasisi za kifedha, kilimo, afya pamoja na juhudi za kuongeza fursa za ajira kwa vijana ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ubelgiji ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya wananchi wa mataifa yote mawili.






Hakuna maoni: