DAR ES SALAAM
Boys Initiative Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imezindua rasmi kaulimbiu ya kitaifa ya Siku ya Mtoto wa Kiume Duniani 2026 inayosema, “Wekeza kwa mtoto wa kiume; kwa kizazi chenye uwajibikaji.”
Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha familia, shule, jamii, taasisi na wadau wa maendeleo kushiriki katika malezi, ulinzi na mwongozo sahihi kwa watoto wa kiume nchini. Pia inalenga kuibua mjadala kuhusu changamoto zinazowakabili watoto wa kiume ikiwemo malezi hafifu, ukosefu wa mwongozo na mazingira hatarishi yanayoweza kuathiri maendeleo yao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mei 16, 2026, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Boys Initiative Tanzania, Dianarose Rweyemamu amesema kaulimbiu hiyo ni mwongozo wa kitaifa unaosisitiza umuhimu wa kuwekeza katika malezi na ustawi wa mtoto wa kiume.
Amesema watoto wa kiume wakipewa malezi bora hukua kuwa wanaume wenye uwajibikaji wanaochangia amani, utulivu na maendeleo endelevu ya taifa.
Wizara imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuhakikisha watoto wa kiume wanakua katika mazingira salama yenye maadili mema, matumaini na fursa za maendeleo.
Kupitia kampeni hiyo, Boys Initiative Tanzania imeeleza itaendelea kuendesha kampeni za uhamasishaji, mijadala ya kijamii, programu za malezi pamoja na shughuli za utetezi wa haki na ustawi wa mtoto wa kiume katika maeneo mbalimbali nchini.

Hakuna maoni: