MCB YAZINDUA UUZWAJI WA HISA, YALENGA KUONGEZA MTAJI NA MIKOPO NAFUU

Na Mwandishi Wetu,

Dar es Salaam. 

Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB) imezindua rasmi mpango wa uuzaji wa hisa stahiki, hatua inayolenga kuimarisha mtaji wa benki hiyo na kupanua utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu, wafanyakazi na wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini.

Akizungumza katika uzinduzi huo leo Mei 6, 2026, Waziri Mkuu Mstaafu Kassim Majaliwa amesema hatua hiyo ni muhimu katika kukuza uwezo wa kifedha wa benki pamoja na kuongeza wigo wa huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Amesema mpango huo unawapa nafasi wanahisa kuongeza umiliki wao huku ukiiwezesha benki kujiimarisha zaidi kifedha na kuwekeza katika huduma za kisasa ikiwemo teknolojia za kidigitali.

“Mbali na kuwa fursa ya uwekezaji, huu ni mchango wa moja kwa moja katika kukuza uchumi wa taifa kupitia taasisi imara ya kifedha,” amesema Majaliwa na kuwataka wanahisa kutumia ipasavyo nafasi hiyo.

Mpango huo unasimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), huku iTrust Finance Limited wakiratibu utekelezaji wake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya MCB, Francis Ramadhani, amesema wanahisa waliokuwepo kwenye rejesta hadi Mei 5, 2026 wanayo haki ya kununua hisa mpya tatu kwa kila hisa moja waliyonayo kwa bei ya Shilingi 110.

Ameeleza kuwa ununuzi wa hisa hizo unafanyika kwa njia ya kidigitali kupitia DSE Hisa Kiganjani, ofisi za Chama cha Walimu Tanzania (CWT) pamoja na matawi ya benki hiyo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, Richard Makungwa, amesema katika miaka mitano iliyopita MCB imepiga hatua kubwa kifedha, ambapo mali zake zimeongezeka kutoka chini ya Shilingi bilioni 30 mwaka 2019 hadi kufikia Shilingi bilioni 98 mwaka 2025.

Ameongeza kuwa amana za wateja pia zimekua kwa kasi kutoka Shilingi bilioni 16 hadi zaidi ya Shilingi bilioni 75, hali inayoonesha kuimarika kwa imani ya wateja na ukuaji wa benki hiyo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.